Ajali ya Kutisha na Supu ya Miguu ya Kuku: Siri ya Kupona ya Andros Townsend
LONDON, England — Supu ya miguu ya kuku inayotumiwa na winga nyota Andros Townsend imekuwa gumzo kubwa duniani kote. Mchezaji huyo amefichua siri ya vyakula vya kipekee alivyovitumia kuponya mwili wake baada ya kukumbwa na ajali ya kutisha ya kugongwa na mashine ya kusawazisha uwanja wa mpira wakati akijiandaa kuingia kipindi cha pili.
Winga huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya England, ambaye kwa sasa anakipiga klabu ya PT Prachuap ya Thailand, alinusurika katika tukio hilo la kushangaza bila majeraha makubwa, na hata kuweza kucheza kama mchezaji wa akiba kipindi cha pili.
Hata hivyo, baada ya mchezo huo, goti lake lilianza kuvimba, jambo lililomlazimisha kuandaa mlo maalum uliomsaidia kurejea haraka.
Katika video aliyoweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, Townsend alieleza kuwa ndani ya saa 24 alizingatia lishe yenye virutubisho hivi muhimu:
-
Supu ya Miguu ya Kuku: Alisema supu hiyo iliyochemshwa taratibu kwa saa nane ilimpatia collagen, gelatin, pamoja na asidi za amino kama glycine na proline zinazojenga kano, mishipa na gegedu.
-
Mayai Sita: Yalimpatia protini bora ya kusaidia ukarabati wa misuli.
-
Vyakula vya Asili (Antioxidants): Alitumia blueberries, mafuta ya zeituni, na kakao mbichi kupunguza uchochezi mwilini.
-
Samaki wa Salmoni & Jibini: Alitumia samaki wenye omega-3 na jibini kwa ajili ya afya ya mifupa na misuli.
-
Matunda yenye Vitamini C: Aliongeza machungwa na kiwi ili kuchochea utengenezaji wa collagen mwilini mwake.
Akihitimisha simulizi yake, mchezaji huyo mwenye miaka 35 alisisitiza kwa hisia kali akisema: “Chakula ni dawa.” Tukio hilo lilimfanya kualikwa kwenye kipindi maarufu cha Piers Morgan Uncensored ili kueleza kisa hicho kizima kilivyotokea.