Yanga Yuchomoa Uzito Kariakoo Dabi Dhidi ya Simba: “Hauamui Ubingwa!”
Uongozi wa klabu ya Yanga umeuchomoa uzito mchezo wao unaosubiriwa kwa hamu wa Kariakoo Dabi dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC, ukisisitiza kuwa mechi hiyo hautakuwa kipimo cha mwisho cha ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Bara.
Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, ameeleza kuwa ingawa pambano hilo linalotarajiwa kupigwa Oktoba 10 ni gumzo kubwa nchini, mabingwa hao watetezi hawapo tayari kuingia kwenye mtego wa kuufanya mchezo huo kuwa ndio uamuzi wa mbio za taji.
Lengo Kuu ni Ubingwa wa 6 Mfululizo
Kamwe amebainisha kuwa lengo kuu la Yanga msimu huu ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya sita mfululizo. Ameikumbusha jamii ya soka kuwa ligi bado ipo hatua za awali kabisa, ikiwa timu zimecheza michezo sita pekee kati ya 30 ya msimu mzima.
“Huu ni mchezo tu wa Dabi. Focus yetu ipo kwenye kutwaa ubingwa mara ya sita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara,” amesema Kamwe.
Akaongeza:
“Kumeshapigwa michezo sita na kwenye ligi kuna michezo 30. Maana yake bado kuna michezo 24 mbele ya kuchezwa. Kwa matokeo ambayo umeyapata sasa hivi, ukiwa hujui mpira yanaweza kukudanganya na ukaamini tayari bingwa anaweza kujulikana kwa michezo sita tu.”
“Ni Pointi Tatu Tu, Sio Uamuzi wa Bingwa”
Licha ya kukiri kuwa Simba ni mshindani wao wa karibu kwenye msimamo wa ligi, Kamwe amesisitiza kuwa matokeo ya Dabi hiyo hayatatoa picha ya nani atakuwa bingwa mwisho wa msimu.
“Ndiyo, tuna mechi mwezi ujao. Ni ligi ndogo ndani ya ligi dhidi ya Simba na ni mshindani ambaye tumezizidi pointi kwenye msimamo. Lakini sio mechi ambayo nasema sasa hii mechi itatoa kwenye mbio za ubingwa, wala sio mechi ambayo itanipa uhakika wa ubingwa. Ni mechi kubwa lakini ni pointi tatu,” amefafanua.
Mechi 23 Zitabaki Mbele
Baada ya kipute hicho cha Kariakoo Dabi kumalizika, Yanga bado itakuwa na kibarua cha michezo 23 kabla ya msimu kufungwa, jambo linalofanya matokeo ya mechi moja kutokuwa na uamuzi wa mwisho.
Kamwe amehitimisha kwa kusema:
“Ukicheza hiyo mechi unabaki na michezo 23 mbele ya kuchezwa. Kwa hiyo naamini focus ya Wanayanga ipo kwenye kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC na sio kwenye mchezo mmoja specific.”