Takwimu za Yanga Zashtua Ligi Kuu: Ubabe wa Kamwe Waacha Gumzo!
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga SC, wameanza msimu huu kwa kishindo kikubwa baada ya kuonyesha kiwango cha juu kinachoendana na takwimu za kuvutia kwenye mechi zao sita za kwanza.
Akizungumzia mwenendo huo, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, ameeleza kuwa mwanzo huu ni miongoni mwa bora na wa kihistoria kuwahi kushuhudiwa klabuni hapo katika misimu ya hivi karibuni. Amesema ubabe wa timu hiyo hauonekani kwenye matokeo ya ushindi pekee, bali unajidhihirisha wazi kupitia takwimu za uwanjani za kufunga, ulinzi na utengenezaji wa nafasi.
“Mwanzo mzuri wa mechi sita za kwanza kuliko misimu mingi ya hivi karibuni. Ukirudi msimu uliopita, msimu tena, msimu tena mpaka ufike enzi za kina Nasreddine Nabi, msimu huu tumekuwa na performance bora in terms of numbers,” amesema Kamwe.
Ulinzi Imara na Utengenezaji wa Nafasi
Mbali na kuongoza msimamo na kufunga mabao mengi, Yanga imesimamaara nyuma kwa kuruhusu mabao machache sana. Kamwe aliongeza kuwa kikosi hicho kimekuwa na wastani mzuri wa kupiga pasi na ndiyo timu iliyoshambuliwa kwa uchache zaidi kwenye Ligi Kuu hadi sasa.
Licha ya ukuta wao kuwa mgumu kupenya, safu ya ushambuliaji nayo imekuwa moto wa kuotea mbali. Yanga inatengeneza wastani wa zaidi ya nafasi nane za wazi za kufunga mabao katika kila mchezo. Uwezo huu ulionekana bayana hata walipocheza wakiwa pungufu kwa zaidi ya dakika 65 dhidi ya Geita Gold.
Mafanikio haya yanatajwa kuchangiwa na kazi kubwa inayofanywa na benchi la ufundi chini ya kocha Manqoba Mngqithi, pamoja na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya viongozi, wachezaji na mashabiki wao.