Makonda Atoa Neno Zito kwa ‘Content Creators’, Awapa Michongo ya Sh2 Bilioni!
Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ametoa pongezi za dhati kwa watengeneza maudhui mtandaoni (Content Creators) nchini kwa mchango wao mkubwa wa kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Makonda amekiri kuwepo kwa changamoto miongoni mwa baadhi ya watengeneza maudhui, lakini amesisitiza kuwa wengi wao wanafanya kazi nzuri na ya weledi inayodhihirisha umuhimu wao kwa taifa letu.
“Niwapongeze sana kwa kazi kubwa mnayoifanya. Siwezi kuwahukumu wote nikiona wachache wanaenda kombo. Ni sawa na kuwa na watoto saba; mmoja wenu anaweza kwenda kinyume hadi ukajiuliza kama kweli anatoka kwenye familia hii,” alifafanua Makonda.
Sambamba na pongezi hizo, Makonda ametumia fursa hiyo kuwakumbusha na kuwahamasisha wasanii mbalimbali nchini kuchangamkia fursa ya Shilingi bilioni 2. Kiasi hiki kimetengwa maalum kwa ajili ya kutoa hamasa na kukuza kazi zao za sanaa, hivyo wasanii wanapaswa kujitokeza kunufaika na mirabaha hiyo.