Uhamiaji FC Ligi Kuu Zanzibar
Michezo Bongo

Uhamiaji FC Yapokea Milioni 2 Baada ya Kuichapa Raskazone ZPL!

Vardo September 25, 2026 2:25 pm

Timu ya soka ya Uhamiaji FC imeendelea kupokea hamasa kubwa baada ya kukabidhiwa Shilingi Milioni 2 kufuatia muendelezo wao mzuri wa matokeo katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu.

Fedha hizo zilikabidhiwa Septemba 24, 2026, na Mwenyekiti wa timu hiyo ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji, Ali Juma Abdulkadir, kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan. Zawadi hiyo imetolewa mara baada ya Uhamiaji FC kuichapa Raskazone bao 1-0 na kufikisha jumla ya mabao 10 katika mechi tano walizocheza.

Gharama hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Kamishna Mkuu, Hassan Ali Hassan, ambaye aliahidi kununua kila bao litakalofungwa na timu hiyo ili kuongeza morali na hamasa kwa wachezaji na benchi la ufundi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hiyo, Abdulkadir alisema:

“Tunafanya hivi kuongeza juhudi na hamasa kwa wachezaji wetu pamoja na benchi la ufundi ili kufikia malengo ya timu bila kuchoka.”

Kwa upande wake, Nahodha wa Uhamiaji FC, Ahmed Ali ‘Salula’, alishukuru uongozi na wadau kwa ushirikiano na hamasa wanayoitoa. Aliahidi kuwa wachezaji wataendelea kupambana uwanjani na hawatawaangusha mashabiki na viongozi wao.

Hivi sasa, Uhamiaji FC inaongoza kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar baada ya kushinda mechi zote tano, ikifunga mabao 10 na kuruhusu bao moja pekee, ikiwa na jumla ya pointi 15.

UEFA Yaonya: Usajili wa Ligi Kuu England Unaharibu