Steve Barker Simba SC
Simba SC

Steve Barker Aweka Wazi Mipango ya Simba SC Afrika Kusini Kuelekea Dabi ya Kariakoo

Vardo September 26, 2026 10:14 am

Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameweka wazi kuwa kambi ya siku 10 wanayoiweka nchini Afrika Kusini si safari ya mapumziko, bali ni mchakato mzito wa kukisuka upya kikosi chake tayari kwa pambano la Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga SC.

Simba SC ilielekea nchini Afrika Kusini tangu Alhamisi, Septemba 24, 2026, mara baada ya kumaliza mapumziko ya siku saba kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC katika Mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Barker ameeleza kuwa kambi hiyo itampa fursa ya kufanya kazi kwa ukaribu na wachezaji wake katika mazingira tulivu. Anapanga kutumia muda huo kurekebisha makosa ya kiufundi na kuimarisha mifumo kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa maandalizi ya mwisho kuelekea Dabi inayotarajiwa kuchezwa Oktoba 10.

Mapumziko haya ya kalenda ya FIFA yamekuwa fursa muhimu kwa kocha huyo kujenga utayari wa kimwili na kiakili ndani ya kikosi. Barker anataka kuongeza uelewano baina ya wachezaji kwenye mfumo wake mpya wa uchezaji na kujenga utulivu wa juu utakaowapa ushindani mkubwa.

Mbali na mazoezi magumu, Wekundu wa Msimbazi wanatarajiwa kucheza michezo kadhaa ya kirafiki nchini humo ili kuendelea kuweka wachezaji kwenye mdundo wa ushindani wakati ligi ikiwa imesimama.

Kwa hesabu za Steve Barker, maandalizi ya kuikabili Yanga hayataanzia Dar es Salaam bali yameshaanza Sauzi. Siku hizi 10 za jasho na mechi za kirafiki ndizo zitakazojenga Simba ya ushindi itakayoshuka uwanjani Oktoba 10 kukamilisha kazi moja tu—kuondoka na alama tatu muhimu.

TAKWIMU ZASEMA NINI? Stars Ilitawala, Guinea-Bissau Ikaua kwa Ufanisi Yanga Waipiga Dongo Simba Kambi ya Afrika Kusini: “Tukutane Uwanjani”