Simba vs Yanga Dabi ya Kariakoo
Yanga SC

Yanga Waipiga Dongo Simba Kambi ya Afrika Kusini: “Tukutane Uwanjani”

Vardo September 26, 2026 10:21 am

Wakati miamba ya soka nchini, Simba SC, ikiwa imeweka kambi ya siku 10 nchini Afrika Kusini kujiandaa na pambano likubwa la Dabi ya Kariakoo, baadhi ya viongozi ndani ya Yanga SC wameanza kuwatupia dongo la kimyakimya wapinzani wao.

Simba wametumia mapumziko haya ya kalenda ya FIFA kusafiri hadi Afrika Kusini kwa ajili ya kuweka mazingira tofauti ya maandalizi pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki kabla ya kurejea nchini kuwakabili Yanga kwenye mchezo utakaopigwa Oktoba 10, mwaka huu.

Hata hivyo, hatua hiyo imeibua mjadala mzito miongoni mwa wadau wa soka na viongozi wa Yanga. Mmoja wa mabosi wa zamani wa Yanga aliyezungumza na vyombo vya habari ameweka wazi kuwa safari hiyo ya mbali haitawapa Simba faida yoyote dhidi yao.

“Tumesikia wenzetu wanakwenda Afrika Kusini. Acha waende wakimaliza kuzuruka, tukutane Uwanja wa Uhuru au kokote watakapopataka. Tutacheza sisi tukiwa tayari, hakuna shida kabisa,” alisema bosi huyo.

Akiendelea kufafanua, kiongozi huyo alisema Yanga imekuwa ikifanya maandalizi yake kwa utulivu mkubwa katika kambi yao iliyopo Kigamboni na haina mpango wa kubadilisha mkakati huo kwa sababu tu Simba wameenda nje ya nchi.

“Yanga huko nyuma ndio tulikuwa na mambo ya kwenda mbali, lakini tumekutana na Simba mara nyingi sana na tumewafunga. Tumekuwa tukitokea Kigamboni mara nne na tumeshinda, hatuna sababu ya kuchosha wachezaji wetu,” aliongeza.

Wakati Simba ikiwa Afrika Kusini, benchi la ufundi la Yanga limewapa wachezaji wake mapumziko ya siku tisa ili kupumzisha miili kabla ya kurejea kambini kuanza maandalizi kabambe ya Dabi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.

Steve Barker Aweka Wazi Mipango ya Simba SC Afrika Kusini Kuelekea Dabi ya Kariakoo Jabaar Afunguka Siri ya Kutisha Simba SC: “Ukiwa na Chama na Maema Kazi Inakuwa Nyepesi!”