KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema mchezo dhidi ya Azam FC kesho ni miongoni mwa vipimo muhimu ambavyo kikosi chake kinapaswa kuvuka kwa ushindi, akisisitiza kuwa timu hiyo inalenga kufanya vizuri zaidi msimu huu kuliko ilivyokuwa msimu uliopita.
Simba itakuwa ugenini dhidi ya Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho Jumatano, huku Barker akikumbusha kuwa katika hatua kama hii ya msimu uliopita, baada ya kucheza mechi tano, timu yake ilipoteza mchezo dhidi ya wapinzani hao.
Barker amesema kutokana na malengo makubwa ambayo Simba imejiwekea msimu huu, wachezaji wanapaswa kuonyesha kiwango cha juu na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo ya aina hiyo, ambayo ni muhimu kwenye mbio za ubingwa.
“Ni jukumu letu kama tunataka kufikia malengo tuliyojiwekea kwenye ligi. Ni aina ya mechi ambazo tunapaswa kuhakikisha tunaweka kiwango kitakachotupa nafasi kubwa ya kupata pointi zote,” amesema Barker.
Kocha huyo amekiri kuwa Azam ni timu yenye ubora na iliyofanya maboresho katika kikosi chake, licha ya kuondokewa na baadhi ya wachezaji. Amesema hilo linaifanya mechi hiyo kuwa ngumu na inayohitaji Simba kuwa makini katika utekelezaji wa mpango wake.
“Azam ni timu iliyofundishwa vizuri, ina wachezaji wazuri na imeimarisha baadhi ya maeneo. Kila mchezo kati ya Simba na Azam ni mgumu. Ni suala la utekelezaji siku hiyo, kufuata mpango wa mchezo na kushughulikia nyakati muhimu,” amesema.
Barker pia amesisitiza umuhimu wa nidhamu, umakini na hamu ya ushindi, akieleza kuwa kucheza ugenini dhidi ya Azam kunahitaji Simba kutoa kiwango chake cha juu ili kupata matokeo inayoyahitaji.
“Ukitaka mafanikio hayaji kirahisi. Lazima uyafanyie kazi. Kesho tutatoa asilimia 100 kufanya hivyo,” amesema.
Aidha, Barker amesema anaamini wachezaji wake wana kiu ya kumaliza sehemu ya kwanza ya mechi za ligi wakiwa na rekodi nzuri, huku akitaja ushindi dhidi ya Azam kuwa hatua muhimu ya kufunga vyema awamu hiyo kabla ya mapumziko.
Hata hivyo, kocha huyo amesisitiza kuwa kabla ya kufikiria mapumziko, Simba ina dakika 90 za kupambana, akiwataka wachezaji wake kuingia uwanjani wakiwa na umakini, ari na utayari wa kupigania pointi tatu dhidi ya Azam.