Kariakoo Derby: Simba Yaitumia Yanga Salamu Nzito Zikiwa Zimebaki Siku Chache
Mchezo wa watani wa jadi wa Kariakoo Derby uliopangwa kuchezwa Oktoba 10 unapanda joto, huku Klabu ya Simba SC ikituma salamu za mapema na za wazi kwa wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
Salamu hizo zimekuja mara baada ya timu ya wanawake ya Simba Queens kuichapa Yanga Princess mabao 3-0 katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii ya Ligi ya Wanawake Tanzania.
Ahmed Ally Arusha Dongo Kuelekea Oktoba 10
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amebainisha kuwa ushindi huo wa Simba Queens sio tu matokeo ya uwanjani, bali ni ujumbe wa wazi kwa timu ya wanaume ya Yanga kabla ya pambano lao la Oktoba 10.
“Salamu. Hii ni salamu. Mpokee salamu zetu kuelekea Oktoba 10. Tunaamini kilichomkuta Kenge na Mamba kitawakuta. Tuseme Inshallah. Tukutane tarehe 10 mwezi wa 10,” amesema Ahmed Ally kwa kujiamini.
Dokezo la Uwanja na Kambi ya Afrika Kusini
Kuhusu uwanja utakaotumika kwa mchezo huo wa kukata na shoka, Ahmed Ally amewataka mashabiki kukaa tayari kwa taarifa rasmi, akidokeza uwezekano wa mchezo huo kuchezwa nje ya nchi.
“Wanauliza uwanja gani? Uwanja tutawatangazia, bado sijui. Lakini wawe ‘very standby’. Inaweza ikawa kama sio Rwanda. Standby tu,” aliongeza Ahmed.
Wakati huo huo, kambi ya Simba nchini Afrika Kusini inaendelea vizuri. Ahmed amethibitisha kuwa mshambuliaji wao mpya, Ibrahim Doumbia, tayari amewasili kambini na kuanza mazoezi makali ya gym ili kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa michezo ya mwezi huu.
Simba inatarajiwa kurejea nchini Oktoba 3 ikitokea Afrika Kusini baada ya kukamilisha kambi ya siku 10, tayari kabisa kuikabili Yanga kwenye Kariakoo Derby.