Mzigo wa Milioni 120 Wamkimbiza Mwekezaji Tausi FC Baada ya Vichapo Vitatu!
Tausi FC, timu iliyokuwa tishio na kutoa ushindani mkubwa katika Ligi Kuu ya Wanawake msimu uliopita, imeanza vibaya kampeni za msimu huu baada ya kupoteza mechi zake zote tatu za mwanzo, huku ikikumbwa na mtikisiko mkubwa wa kiuongozi.
Klabu hiyo, ambayo awali ilifahamika kama Ukerewe Queens kabla ya kubadilishwa jina baada ya kupanda daraja kutoka Ligi ya Mkoa, ilijipambanua kwa uwekezaji mkubwa uliohusisha makocha wenye uzoefu pamoja na usajili wa nyota wa kimataifa. Hata hivyo, upepo umebadilika ghafla msimu huu kufuatia kujiondoa kwa aliyekuwa akiisimamia timu hiyo kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.
Kibali Kimoja Chaigharimu Klabu Milioni 12
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo, mzigo mkubwa wa gharama za vibali vya kufanyia kazi kwa wachezaji wa kigeni ndio chanzo kikuu cha mkwamo huo. Inaelezwa kuwa kibali cha mchezaji mmoja wa kigeni kinagharimu takriban Shilingi milioni 12.
Wakala wa nyota wa kimataifa wa Tanzania, Clara Luvanga na Aisha Masaka, Anton Maksimov, ndiye anayetajwa kuinunua na kuiendesha timu hiyo, lakini amelazimika kukaa kando baada ya kuona gharama hizo zikizidi bajeti na matarajio yake. Ukiangalia kuwa Tausi FC ina zaidi ya wachezaji 10 wa kigeni, gharama za vibali pekee zinapita Shilingi milioni 120, jambo lililoibua maswali mengi kuhusu uendelevu wa kikosi hicho.
Alliance Girls Yachukua Usimamizi kwa Muda
Kutokana na mkwamo huo wa kifedha na kiutawala, wachezaji wengi wa kigeni wameshindwa kuingizwa kwenye mfumo rasmi wa usajili, hali iliyodhoofisha kikosi chao uwanjani.
“Kuna taarifa kwamba sasa hivi Tausi iko chini ya uangalizi wa Alliance Girls ndio wanaisimamia, lakini wachezaji wengi wa kigeni hawajaingizwa kwenye mfumo. Kwa hiyo, Anton ameiacha kwa sasa kutokana na mzigo mkubwa wa vibali,” kilieleza chanzo kimoja kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo.
Hali hii inaiweka Tausi FC katika wakati mgumu zaidi msimu huu, ikilazimika kujipanga upya kiuchumi na kiufundi ili kunusuru mwenendo wake katika ligi.