Kutoka Gate Crasher Hadi Mamilionea: Safari ya MC Gara B Kwenye U-MC
Kuna watu wanaingia kwenye kazi kwa mlango mkubwa, wengine wanabisha hodi, lakini Godfrey Deogratius Rugarabamu, maarufu kama MC Gara B, yeye alianza kwa kutafuta mwanya wa kuingia ndani ya sherehe hata kama jina lake halikuwepo kwenye orodha ya wageni (gate crasher).
Alifika kwenye harusi kama mwanafunzi anayekwenda darasani—akasikiliza, akatazama na kujifunza kila kilichokuwa kikifanyika jukwaani. Wakati mwingine alijikuta akiingia kama msaidizi wa DJ, huku nyakati nyingine akifanya kazi ya uhudumu wa vinywaji ili tu awe karibu na ma-MC na kuona namna wanavyoendesha shughuli kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Leo hii, MC Gara B ni miongoni mwa majina makubwa na yenye ushawishi kwenye tasnia ya U-MC Tanzania. Hata hivyo, safari yake haikuanza na kamera, umaarufu wala mialiko minene; ilianza na ndoto, kukosa nafasi kwenye vyombo vya habari, na maamuzi ya kugeuza jukwaa la harusi kuwa fursa ya maisha yake.
Elimu ya Ualimu, Lakini Moyo Kwenye Utangazaji
Licha ya kusomea taaluma ya ualimu, moyo wa MC Gara B ulikuwa kwenye utangazaji. Baada ya kukosa ajira kwenye vyombo vya habari, aliamua kutafuta njia mbadala ya kufikia ndoto yake kupitia shughuli za kijamii.
“Nilisomea ualimu lakini nilikuwa na mapenzi makubwa ya utangazaji. Nilipokosa nafasi kwenye TV na redio, nikaona kwenye harusi kuna ma-MC wanafanya vizuri. Nikaanza kuliona jukwaa lile kama TV show yangu mwenyewe,” anasimulia Gara B.
Badala ya kusubiri fursa imfuate, alianza kuzunguka kwenye shughuli mbalimbali ili kufanya utafiti wa soko. Alifanya kazi za umasherie, kusaidia ma-DJ, na wakati mwingine kuingia bila mwaliko ili tu ajifunze kutoka kwa wakali wa kipindi hicho.
Mwonekano na Soko la Karume: Siri ya Kutofautiana
Baada ya kubaini ushindani mkubwa uliokuwepo sokoni, MC Gara B alitambua kuwa kipaji pekee hakikutosha—ilimlazimu kuwekeza kwenye mwonekano wake.
Akiwa na kipato kidogo, alianza kwenda soko la Karume kutafuta suti na makoti ya pamba yenye muonekano wa kipekee ili ajitofautishe na ma-MC wengine.
“Niliona hatuwezi kuendelea kuomba vigelegele na makofi tu. Nikaanza ku-hype nyimbo za wasanii wa ndani na nje wakati maharusi wanaingia. Hapo ndipo watu wakaanza kuona kuna kitu tofauti,” anasema.
Mwaka 2012: Rasmi Kwenye Ajira na Changamoto za Mwanzo
Mwaka 2012 ndio ulikuwa mwanzo wa MC Gara B kuichukulia kazi ya U-MC kama ajira rasmi baada ya kuanza kulipwa. Kipindi hicho alikutana na ma-MC waliokubalika kama Dr. Chen, Anthony Luvanda, Dr. Ndimbo, MC A, Uncle na Kwayu.
Kabla ya kujikita kikamilifu, alilazimika kufanya kazi zaidi ya moja kwa siku:
-
Asubuhi (Saa 1:00 – 8:00 Mchana): Mwalimu wa shule.
-
Mchana: Kazi ya huduma kwa wateja (Customer Care) kampuni ya simu.
-
Usiku: Mfanyakazi kwenye kiwanda cha mabati.
Anakumbuka siku moja alipopata uenyekiti wa sherehe ya mfanyakazi mwenzake, alichukua ruhusa ya ugonjwa (sick sheet) kazini. Hata hivyo, bosi wake naye alihudhuria harusi hiyo na kumkuta Gara B akiwa jukwaani akiendesha shughuli kwa umahiri!
Kwenye hatua za mwanzo, alifanya kazi nyingi bure au kwa malipo madogo ya Sh10,000 hadi Sh20,000 ili tu kupata nauli na kujenga jina lake.
Mitandao ya Jamii na Simu za Dharura Zilivyomnyanyua
Jina la MC Gara B lilianza kukua zaidi kupitia simu za dharura kutoka kwa ma-MC wakubwa waliokuwa wakipata dharura kwenye shughuli walizowekewa booking. Gara B alitumia fursa hizo kuonyesha uwezo wake wa hali ya juu, jambo lililofanya wateja kuanza kumtafuta moja kwa moja.
Pia, hakuwa tayari kuachia kazi zake ziishie ukumbini. Aliwekeza kwenye wapiga picha na video wake binafsi ili kupata maudhui ya haraka na kuyarusha kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na YouTube.
Booking 60 kwa Siku Moja na ‘Pamba’ ya Mamilioni
Hivi sasa, MC Gara B amekuwa miongoni mwa ma-MC wenye maombi mengi zaidi nchini, kiasi cha kupokea hadi booking 60 kwa tarehe moja.
Kuhusu muonekano wake wa sasa, anabainisha kuwa vazi moja analovaa jukwaani kuanzia juu hadi chini (koti, viatu, saa na skafu) halipungui gharama ya Shilingi Milioni 1.
“Mteja halipii MC mmoja tu anayeshika kipaza sauti. Analipia taasisi yenye ofisi, wafanyakazi zaidi ya 20, ushauri nasaha, huduma za picha na video, pamoja na thamani ya chapa yetu,” anafafanua.
Uhusiano na Harmonize na Mafanikio Mengine
MC Gara B amepata fursa ya kuendesha shughuli za mastaa mbalimbali, ikiwemo hafla mbili za uchumba za msanii Harmonize na Kajala. Anamwelezea Harmonize kama mtu anayeheshimu kazi na anayemchukulia kama kaka yake.
Mbali na mafanikio ya kifedha, Gara B anajivunia kujenga mtandao mkubwa wa watu wakiwemo viongozi wa serikali, mawaziri, na maaskofu. Pia, kupitia mpango wake wa ‘UpSkill Class’ anaousimamia na MC Mchoma kwa miaka 7 sasa, ameweza kuwafunda na kuwasaidia ma-MC wengi chipukizi.
Simba Damu na Ushauri Kwa Taifa Stars
Kando na jukwaa la U-MC, Gara B ni mpenzi mkubwa wa mpira wa miguu na mshabiki damu wa Simba SC, akimfagilia golikipa wa zamani Juma Kaseja pamoja na kiungo Clatous Chama.
Akiitazama Timu ya Taifa (Taifa Stars) kuelekea mashindano ya AFCON, amewasihi TFF, Wizara ya Michezo na wadau wote kuwekeza kwenye maandalizi ya dhati na kuweka kando migogoro au siasa zisizo na tija.