Michael Joseph wa Mashujaa
Michezo Bongo

Rekodi Zao! Kwa Nini Wafungaji Bora wa Ligi Kuu Zanzibar Wanafeli Ligi Kuu Bara?

Vardo October 1, 2026 9:30 am

Mnamo Julai 20, 2026, uongozi wa Mashujaa FC ulimtambulisha rasmi mshambuliaji Michael Joseph ili kuongeza nguvu kikosini kwa msimu wa 2026/2027, akitokea kikosi cha KVZ kinachoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Michael alijiunga na Mashujaa FC akiwa na sifa kibao, kwani ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025/2026 baada ya kupachika mabao 21 katika mechi 29 (dakika 2320). Pia alitoa asisti 8 na kuhusika kwenye jumla ya mabao 29, kiwango kilichoipatia KVZ ubingwa wa ZPL kwa pointi 67.

Hata hivyo, Michael anakabiliwa na mtihani mzito wa kuvunja ‘mwiko’ wa washambuliaji wanaotokea visiwani humo kushindwa kutamba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC Premier League). Hapa tunawazia baadhi ya wafungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar waliotua Bara na kupata wakati mgumu:

1. Maabad Maulid (KVZ kwenda Coastal Union)

Maabad Maulid alijiunga na Coastal Union mnamo Julai 11, 2022, akitokea KVZ. Alikuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo Zanzibar—msimu wa 2020/2021 (mabao 17) na 2021/2022 (mabao 21).

Licha ya rekodi hizo, Maabad amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka Ligi Kuu Bara:

  • 2022/2023: Mabao 4

  • 2023/2024: Mabao 3

  • 2024/2025: Mabao 5

  • 2025/2026: Mabao 10 (Msimu wake bora zaidi Bara)

  • 2026/2027: Mabao 3 (hadi sasa)

2. Abdallah Idd ‘Pina’ (Mlandege kwenda Pamba Jiji)

‘Pina’ alitua Pamba Jiji ya Mwanza Agosti 7, 2025, kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mlandege. Msimu wa 2024/2025 alikuwa mfungaji bora Zanzibar baada ya kufunga mabao 21 na asisti 12 katika mechi 22 pekee.

Licha ya matarajio makubwa, Pina alishindwa kufunga bao hata moja Ligi Kuu Bara akiwa na Pamba Jiji, hali iliyopelekea kupelekwa Muembe Makumbi City kwa mkopo na baadaye kurejea ZPL kujiunga na KVZ kwa msimu wa 2026/2027.

3. Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’ (JKU kwenda Fountain Gate)

Baada ya kuondoka kwa Seleman Mwalimu ‘Gomez’, Fountain Gate ilimsajili Gonda katika dirisha dogo la Januari 2025 kutoka JKU ili kuziba nafasi hiyo.

  • 2024/2025: Alimaliza msimu bila bao lolote Bara.

  • 2025/2026: Alifunga bao moja pekee la Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji (Oktoba 17, 2025).

Kiwango hicho kilisababisha kuachwa na Fountain Gate kabla ya kurejea visiwani kujiunga na KVZ kwa msimu wa 2026/2027.

4. Ibrahim Hamad Hilika (Zimamoto kwenda Bara)

Hilika alipata umaarufu mkubwa akiwa na Zimamoto ya Zanzibar ambapo alikuwa mfungaji bora mara mbili:

  • 2016/2017: Mabao 33 (19 Unguja, 14 Hatua ya 8 bora)

  • 2019/2020: Mabao 20

Licha ya uwezo huo wa kupachika mabao, alipokuja Ligi Kuu Bara na kuzichezea Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar, na TRA United, alipata ufinyu mkubwa wa nafasi ya kucheza na kushindwa kuonyesha makali yake, hadi TRA United walipositisha mkataba wake msimu wa 2026/2027.

5. Yassin Mgaza (KMKM kwenda Dodoma Jiji)

Yassin Mgaza alikuwa mfungaji bora wa ZPL msimu wa 2022/2023 akiwa na KMKM baada ya kuhusika kwenye mabao 25 (mabao 17, asisti 8).

Dodoma Jiji ilimsajili kwa ajili ya msimu wa 2023/2024, lakini takwimu zake zimekuwa za kusuasua:

  • 2023/2024: Mabao 3

  • 2024/2025: Bao 1

  • 2025/2026: Mabao 3

  • 2026/2027: Bao 1 (hadi sasa)

Je, Michael Joseph Ataweza Kuvunja Mwiko Mashujaa FC?

Hadi sasa katika msimu wa 2026/2027, Michael Joseph bado hajafungua akaunti yake ya mabao Ligi Kuu Bara. Pia anakabiliwa na ushindani mkali wa namba kutoka kwa George Mpole (mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara 2021/2022) aliyesihiwa kujiunga na Mashujaa FC akitokea Tanzania Prisons.

Je, unadhani tatizo ni tofauti ya mbinu na ushindani kati ya ZPL na NBC Premier League, au wachezaji wenyewe wanakosa uvumilivu? Toa maoni yako hapa chini!

Simba Queens Yaitandika Yanga Princess 3-0, Ujumbe Mzito Kabla Ya Ligi Na Dabi