Simba SC Afrika Kusini
Simba SC

Patrick Rweyemamu Afichua Siri ya Mafanikio Kambi ya Simba SC Afrika Kusini

Vardo October 2, 2026 8:57 am

MENEJA wa Simba, Patrick Rweyemamu, amesema kambi ya timu hiyo nchini Afrika Kusini imefanikiwa kwa kiwango kikubwa, akifichua kuwa zaidi ya asilimia 80 hadi 90 ya mipango iliyowekwa imetekelezwa, huku akisisitiza kikosi hicho kiko tayari kurejea kwenye ushindani baada ya mapumziko ya FIFA.

Rweyemamu amesema Simba imebakiza siku mbili kabla ya kurejea Dar es Salaam, huku akieleza kuwa pamoja na changamoto ndogo iliyojitokeza kwenye idadi ya wachezaji, mambo mengine muhimu yaliyolengwa kambini yameenda vizuri, hususan katika eneo la mazoezi, umakini wa wachezaji na utekelezaji wa mipango ya benchi la ufundi.

“Tumebakisha siku mbili, Jumapili tunatarajia kurejea Dar es Salaam Tanzania. Kambi ilikuwa na mafanikio makubwa. Inaweza ikawa kulikuwa na changamoto kidogo kwenye kukamilisha idadi ya wachezaji, lakini kile tulichokipanga kwa asilimia 80 hadi 90 tumeweza kufanikiwa,” amesema Rweyemamu.

Amesema kiwango cha umakini wa wachezaji kimekuwa kikubwa katika kipindi chote cha kambi, huku mazoezi na mipango ya kiufundi ikitekelezwa kwa lengo la kukiandaa kikosi kwa michezo ijayo baada ya mapumziko ya FIFA.

“Umakini wa wachezaji umekuwa mkubwa, mazoezi na mipango imefanikiwa, vilevile game plan kama tunavyokwenda, kwa sababu hii ni muendelezo wa pale tulipoishia kwenye pre-season iliyopita ili tuweze kufanya vizuri kwenye mechi zetu ambazo tunakuja nazo baada ya mapumziko ya FIFA,” amesema.

Kwa upande wa michezo ya kirafiki iliyochezwa kambini, Rweyemamu amesema haikulenga matokeo pekee, bali ilikuwa sehemu ya maandalizi ya kiufundi na kurejesha utimamu wa miili ya wachezaji kabla ya kurejea kwenye ushindani.

“Mechi tunazocheza ni za kiufundi zaidi, sio za kirafiki kwa maana ya kirafiki. Miili inafunguka na wachezaji wanakuwa wepesi. Haya ni muendelezo wa kile ambacho tulifanya kwenye pre-season iliyopita,” amesema.

Akizungumzia utayari wa kikosi, Rweyemamu amesema anaona dalili nzuri kwa wachezaji, akisisitiza kuwa wamejenga ari na utayari wa kupambana kwenye michezo inayofuata.

“Maana yake tuko tayari. Tuko tayari na hata ukiangalia wachezaji katika nyuso zao unaona kabisa wako tayari katika kupambana.

Mimi kama benchi la ufundi nikiwa mmoja wapo naamini kwamba kuanzia sasa na kuendelea tunaweza tukaongeza kitu kutoka pale tulipoishia,” amesema.

Rweyemamu amesema Simba inalenga kupiga hatua zaidi baada ya kambi hiyo, akiamini maandalizi waliyofanya Afrika Kusini yataisaidia timu hiyo kurejea kwenye ushindani ikiwa na nguvu na mpango wa kupata matokeo mazuri.

“Kama tulikuwa namba moja, sasa hivi tunaenda namba mbili. Mwisho wa siku tutapata matokeo mazuri,” amesema.

Simba Queens 3-0 Yanga Princess: Mbinu na Sababu Zilizopelekea Yanga Kufungwa Ngao ya Jamii Ratiba ya Yanga Oktoba: Mzigo Mzito, Dabi ya Kariakoo na Mechi Zote za Ligi Kuu