Amini Africa Afunguka Mazito: Siri ya ‘Robo Saa’, Ruge Mutahaba na Mapenzi na Linah
MWANAMUZIKI nguli wa Bongo Flava, Amini Africa (zamani Amini THT), amefunguka mazito kuhusu safari yake ya muziki, ukimya wake wa muda mrefu, mchango wa marehemu Ruge Mutahaba, pamoja na ukweli juu ya uvumi wa kuwa na bifu na Barnaba Classic kisa Linah Sanga.
Akizungumza maeneo ya Mwananyamala Komakoma jijini Dar es Salaam, Amini amebainisha kuwa ukimya wake haukuwa wa kuacha muziki, bali alikuwa bize kuwekeza katika kuijenga bendi yake inayojulikana kama Amini Band.
Sababu ya Ukimya na Mipango Mipya
Amini ameeleza kuwa muda mwingi aliokuwa haonekani kwenye vyombo vya habari alikuwa akifanya maonyesho ya jukwaani (Live Performances) kupitia Amini Band.
“Nilikuwa najenga Amini Band. Tunafanya shughuli mbalimbali na kutumbuiza kwenye matukio tofauti. Kwa sasa nimeamua kurudi rasmi kama msanii binafsi ili kuongeza thamani yangu sokoni na ya bendi pia,” alisema Amini.
Kwa sasa msanii huyo anatamba na nyimbo zake mpya za mapenzi kama ‘Kaisari’ na ‘Unguja’, huku akiandaa video zake na kutangaza ujio wa kazi mpya yenye ladha ya mtindo wa Singeli.
THT Ilimtoa Kwenye Hip Hop Hadi Kuwa Mwimbaji
Historia ya Amini kwenye muziki ilianzia mbali. Kabla ya kujiunga na kituo cha Tanzania House of Talent (THT) mwaka 2004, alikuwa akifanya muziki wa Hip Hop na alitoa wimbo wake wa kwanza mwaka 2002.
Amini anasema muziki upo kwenye damu ya familia yao, kwani dada zake walikuwa wakiimba kwaya na marehemu kaka yake mkubwa, Bahati Mwenyemkumpila, alikuwa mpiga gitaa la solo. Baada ya kuelekezwa THT na msanii Vumilia, ndipo mtazamo wake ulipobadilika na kuanza kuimba Bongo Flava na Live Band.
Mchango wa Ruge Mutahaba Kwenye Maisha Yake
Anapokumbuka safari yake ya THT, Amini amemwezea marehemu Ruge Mutahaba kama kiongozi aliyekuwa na maono makubwa na aliyetenda kama mzazi.
“Ruge alikuwa zaidi ya bosi, alikuwa kama mzazi. Alikuwa anatusikiliza nyimbo kabla hazijatoka na kutuambia kama ni hit au la. Pia alitusaidia kwenye changamoto za maisha kama kodi na chakula, huku akitufundisha kujitegemea,” alieleza.
Siri Nzito Inayojificha Nyuma ya Wimbo ‘Robo Saa’
Wimbo maarufu wa ‘Robo Saa’ uliompa heshima kubwa Amini na Barnaba una historia ya kipekee.
Amini amefichua kuwa wazo la wimbo huo lilitokana na mkasa wa kweli wa rafiki yake aliyeitwa Mtima Salehe, aliyekuwa ameumizwa vibaya na mapenzi hadi kutamani kufariki dunia baada ya kuachwa na mpenzi wake.
Miondoko (beat) ya wimbo huo ilitengenezwa na Moza Kinanda kwa kutumia kinanda cha Yamaha, huku Amini akirekodi M-Lab na Barnaba akirekodi Enrico.
Ukweli Kuhusu Bifu na Barnaba Kisa Linah
Kuhusu uvumi uliodumu kwa miaka mingi kwamba alikuwa na ugomvi na Barnaba kisa Linah Sanga, Amini ameweka wazi kuwa haijawahi kutokea bifu kati yao.
Alifafanua kuwa wakati huo yeye alikuwa kwenye mahusiano na Linah, huku Barnaba akiwa na mpenzi wake aliyeitwa Lulu—ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Linah. Tofauti hizo ndizo zilizowafanya mashabiki wachanganye mambo.
Pia, amewasihi mashabiki na vyombo vya habari kuacha kumwita majina ya zamani kama “Amini wa Linah” au “Amini wa Robo Saa”, na badala yake wamtambue kwa jina la Amini Africa—jina linaloakisi ladha ya Kiafrika katika sauti na muziki wake.
Kazi Mpya na Barnaba na Ndoto za Baadaye
Amini amethibitisha kuwa tayari amerekodi wimbo mpya na Barnaba (ambaye anamuita pacha wake) na kwa sasa upo kwenye hatua za mwisho za mixing na mastering chini ya mtayarishaji Duly Thomas. Pia anatamani kufanya kolabo na wasanii kama Marioo, Harmonize, Alikiba na J Melody.
Katika mipango yake ya miaka mitano ijayo, Amini anatarajia kuanzisha chuo cha muziki (Music College) ili kuwasaidia vijana wenye vipaji kujiajiri kupitia sanaa.
Ushabiki Wake Kwa Simba SC na Clatous Chama
Nje ya jukwaa la muziki, Amini Africa ni shabiki mkubwa wa klabu ya Simba SC. Kuhusu mechi za Dabi kati ya Simba na Yanga, anaamini ni michezo migumu isiyotabirika.
Akimzungumzia mchezaji anayemkubali zaidi, Amini alimtajia Clatous Chama akisema: “Anaweza akakosea hata mara 20, lakini mara ya 21 akakupa furaha. Yule jamaa ana akili kubwa sana ya mpira.” Alimalizia kwa kutoa rai kwa mashabiki kuwapa muda wachezaji wapya na kuweka msisitizo kwenye kauli mbinu ya “Simba Nguvu Moja”.