Ratiba ya Ligi Kuu Bara Leo: Azam, Kaze na Mbeya City Kazini!
Msisimko wa Ligi Kuu Tanzania Bara unarejea kwa kishindo leo baada ya kupisha mapumziko ya takribani wiki tatu ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Jumla ya mechi nne za kukata na shoka zitapigwa kwenye viwanja mbalimbali nchini, huku kila timu ikisaka pointi tatu muhimu.
Tazama mchanganuo kamili wa mechi zote za leo:
1. Fountain Gate vs JKT Tanzania (Saa 8:00 Mchana)
-
Uwanja: Sheikh Amri Abeid, Arusha
Kibarua cha kwanza kitakuwa jijini Arusha ambapo Fountain Gate, inayokamata nafasi ya 14 ikiwa na pointi 4, itakuwa nyumbani kuwakaribisha maafande wa JKT Tanzania walio katika nafasi ya 10 na pointi zao 7.
Fountain Gate inaingia uwanjani ikitafuta ushindi wa pili msimu huu baada ya kucheza mechi 6 (kushinda 1, sare 1 na kupoteza 4). Kwa upande wa JKT Tanzania, wao wameshinda mechi 2, sare 1 na kupoteza 3.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana zilitoka sare ya mabao 2-2 Mei 21, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
2. Mbeya City vs Kagera Sugar (Saa 10:15 Alasiri)
-
Uwanja: Sokoine, Mbeya
Mechi hii inasubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na ujio wa Kocha Mkuu mpya wa Kagera Sugar, Mrundi Cedric Kaze, aliyechukua mikoba ya Juma Kaseja. Kagera Sugar ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 2 pekee baada ya kucheza mechi 6 bila ushindi (sare 2, vipigo 4).
Kaze amebainisha kuwa ametumia siku 10 kurekebisha makosa:
“Ni mechi ngumu lakini muhimu sana kwetu katika kupambania pointi tiga zitakazoturejesha vizuri. Tunajua Mbeya City wako vizuri msimu huu, lakini tutapambana.” — Cedric Kaze.
Kwa upande wa Mbeya City inayoshika nafasi ya 6 ikiwa na pointi 10, Kocha Salum Mayanga amesema wanaingia uwanjani kwa nidhamu ya hali ya juu wakitambua mabadiliko ya kiufundi yaliyofanywa na wapinzani wao.
3. Dodoma Jiji vs Singida Black Stars (Saa 1:00 Usiku)
-
Uwanja: Jamhuri, Dodoma
Dodoma Jiji (nafasi ya 7, pointi 10) itakuwa na kibarua cha kulipiza kisasi dhidi ya Singida Black Stars (nafasi ya 4, pointi 10). Timu hizi zinalingana pointi lakini zinatofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Dodoma Jiji inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 5-0 ilichokipata mara ya mwisho zilipokutana Juni 17, 2026 mjini Singida.
4. Coastal Union vs Azam FC (Saa 3:00 Usiku)
-
Uwanja: Mkwakwani, Tanga
Raha ya soka la usiku itamalizika jijini Tanga. Coastal Union (nafasi ya 11, pointi 7) itawakaribisha matajiri wa Azam FC wanaoshika nafasi ya 3 wakiwa na pointi 14.
Azam FC inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika Uwanja wa Mkwakwani Juni 26, 2026, yaliyofungwa na Landry Zouzou na Feisal Salum ‘Fei Toto’.