Kocha wa Alliance Girls Afichua Siri ya Timu Kabla ya Ligi Kuu
Kocha wa Alliance Girls, Sultan Juma, amefichua kuwa timu hiyo inaendelea kufanyia kazi kwa karibu mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi za kirafiki, huku eneo la ulinzi likiwa ni kipaumbele kikubwa cha kuboreshwa kabla ya kurejea kwa Ligi Kuu ya Wanawake.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Juma alieleza kuwa wanatumia michezo ya kirafiki kupima uwezo halisi wa wachezaji na kubaini maeneo yanayohitaji marekebisho ili kuhakikisha kikosi kinakuwa imara na cha ushindani mkubwa ligi itakaporejea.
Timu hiyo ilicheza mechi za kirafiki dhidi ya wapinzani mbalimbali wakiwemo Bilo Queens na Iboma Queens, ambapo walipata fursa ya kujenga uwezo wa wachezaji na kuwapa uzoefu wa ugumu wa ligi inayokuja.
“Tumecheza mechi tatu za kirafiki, ikiwemo dhidi ya Bilo Queens, Iboma Queens na tumewaelekeza vijana namna gani ligi ilivyo ngumu. Tunatumia michezo hiyo kuona maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi,” amesema Juma.
Ameongeza kuwa pamoja na mazuri yaliyopatikana, bado kuna changamoto kwenye eneo la ulinzi ambazo benchi la ufundi linazishughulikia kwa karibu ili kupunguza makosa ya wazi wakati wa michuano hiyo.
Hata hivyo, kocha huyo alibainisha kuwa bado hawajapata taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka husika kuhusu tarehe halisi ya kuanza tena kwa ligi hiyo, licha ya awali kuambiwa ingeanza Oktoba 23.