Terence Crawford Awa Mlezi Rasmi wa Ligi ya Ngumi Dunda Tanzania!
Bingwa wa zamani wa dunia katika ndondi za kulipwa, Terence “Bud” Crawford, amekubali rasmi kuwa mlezi wa Ligi ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, Dunda, inayolenga kuibua na kukuza vipaji vya mabondia chipukizi nchini.
Crawford alishiriki uzinduzi wa ligi hiyo pamoja na mchujo wa mabondia wanaowania nafasi za kushiriki mashindano hayo, yanayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ligi hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) na kituo cha redio cha Times FM, ikiwa na lengo la kuimarisha maendeleo ya mchezo wa ngumi na kuwapa mabondia wenye vipaji jukwaa la kujitangaza ndani na nje ya nchi.
Safari na Maandalizi ya Dunda
Crawford, staa wa Marekani aliyejizolea mataji ya dunia katika uzani tofauti na kumaliza rekodi yake bila kupoteza pambano lolote, alishiriki uzinduzi wa Dunda uliofanyika Mei 25, 2026, jijini Dar es Salaam.
Baadaye, Oktoba 3 na 4 mwaka huu, alishiriki pia katika shughuli za mchujo wa mabondia waliokuwa wakiwania nafasi za kuingia kwenye ligi hiyo, ambapo mamia ya washiriki walijitokeza kuonyesha uwezo wao mbele ya majaji wenye uzoefu.
Akizungumzia hatua hii, Makamu wa Rais wa TPBRC, Jacob Mbuya, alisema:
“Kwa nafasi yake kama mlezi na balozi wa kimataifa wa Dunda, Crawford anatarajiwa kusaidia kuhamasisha na kuendeleza vipaji vya mabondia wanaochipukia.”
Mbuya aliongeza kuwa maandalizi yamefika pabaya baada ya kukamilika kwa mchujo, na majina ya mabondia waliofaulu yatatangazwa Novemba mwaka huu sambamba na ratiba rasmi ya mapambano.
Rekodi ya Kutisha ya Terence Crawford
Ujio wa Crawford unaleta hamasa kubwa kutokana na ukubwa wa jina lake kwenye ulimwengu wa ngumi. Rekodi yake ya kutopoteza pambano lolote na kutwaa mikanda katika uzani tofauti kumemfanya kuwa mmoja wa mabondia bora kuwahi kutokea.
Miongoni mwa matukio yake makubwa ni ushindi wake wa kihistoria dhidi ya Saul “Canelo” Alvarez mnamo Septemba 13, 2025, ambapo alishinda kwa pointi baada ya raundi 12, na kufikisha ushindi katika mapambano yake yote 42 (akiwamo 31 kwa KO) tangu aanze ngumi za kulipwa Machi 2008. Amewahi pia kuwashinda vigogo kama Errol Spence Jr, Amir Khan, Shawn Porter, na Kell Brook.
Wadau wa ngumi nchini wanaamini kuwa uwepo wa Crawford utawapa mabondia wa Kitanzania mwanga na fursa ya kupiga hatua hadi kwenye medani za kimataifa.