Clara Luvangaangaza Marekani: Atishia Kuiteka NWSL, Aikataa Benchi Washington Spirit!
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Clara Luvanga, anaendelea kuandika historia ya kipekee nchini Marekani baada ya kuaminiwa na kuanza katika kikosi cha kwanza cha Washington Spirit kilichoibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Gotham FC, Oktoba 17.
Clara, ambaye ndiye mchezaji pekee kutoka Tanzania anayepiga tizi kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake Marekani (NWSL), alicheza kwa dakika 79 ngumu kabla ya kupisha nafasi yake. Hatua hii inaonyesha wazi jinsi nyota huyo anavyozidi kujitengenezea nafasi ya kudumu katika kikosi hicho kikubwa.
Safari ya mafanikio ya Clara ndani ya kikosi hicho inazidi kushika kasi baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika mechi zake za mwisho:
-
Mechi ya Kwanza (Septemba 26): Alicheza dakika 24 akitokea benchi dhidi ya Angel City FC.
-
Mechi ya Pili (Oktoba 4): Aliingia kipindi cha pili na kuandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao Ligi Kuu ya Marekani kwenye ushindi wa 3-2 dhidi ya Houston Dash.
-
Mechi ya Tatu (Oktoba 17): Alianza moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na kuisaidia timu kuibuka na ushindi dhidi ya Gotham FC.
Ushindani wa namba ndani ya Washington Spirit ni mkubwa, lakini kwa kasi hii, Clara Luvanga anazidi kujithibitisha kama lulu mpya ya soka la wanawake kutoka Tanzania inayokwenda kuandika historia kubwa kimataifa.