Kocha wa Tusker Atapaa Dar! Achimba Mkwara Mzito kwa Singida Black Stars
Kikosi cha Tusker FC ya Kenya kimetua nchini Tanzania tayari kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Singida Black Stars, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Mfaransa Julien Mette, akituma salamu nzito kwa wapinzani wao.
Mchezo huo wa kusisimua umepangwa kupigwa keshokutwa Jumapili saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam. Tusker inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza, lililofungwa na Mkongomani Jeancy Mboma Kinda kunako dakika ya 52.
Akizungumzia mchezo huo wa usiku wa Jumapili, Julien amesema kuwa licha ya kupoteza nyumbani nchini Kenya, hawajaja kinyonge Tanzania na wanaamini wenyeji wao watacheza kwa kushambulia tofauti na mbinu za kujilinda walizozitumia ugenini.
“Sisi tulikuwa bora lakini tulipoteza, wapinzani wetu walitumia mbinu za kujilinda na kutunyima nafasi ya kuwashambulia. Mechi ya marudiano itakuwa ngumu, ila tunatakiwa kutengeneza zaidi mashambulizi ya moja kwa moja. Tunaamini tutaibuka na ushindi na kufuzu hatua inayofuata,” amesema Julien.
Kocha huyo ameongeza kuwa kufungwa bao 1-0 hakujakatisha tamaa ndoto zao za kutinga hatua ya makundi, akibainisha kuwa tofauti ingekuwa ni mabao 2-0. Hivyo, amewatoa hofu mashabiki wao kuwa wamefanyia kazi kubwa safu ya ushambuliaji ili kurekebisha makosa ya mchezo uliopita.
Julien amekiri kuwa kilichowagharimu katika mchezo wa kwanza ni kushindwa kutumia vizuri nafasi walizozipata, jambo ambalo wamelipatia ufumbuzi kupitia wachezaji wao wenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kutawala uwanja.