Nathaniel Chilambo
Simba SC

Siri ya Nyota wa Simba SC Nathaniel Chilambo Kuwasha Moto Yashtua!

Vardo October 23, 2026 8:49 am

BEKI wa pembeni wa Simba SC, Nathaniel Chilambo, amefichua siri iliyopo nyuma ya kiwango chake bora kinachoendelea kuwavutia mashabiki wa Wanasimba, akitaja kufuata maelekezo ya benchi la ufundi chini ya Kocha Steve Barker pamoja na kutumia ubunifu wake binafsi uwanjani kuwa silaha yake kuu.

Akizungumzia mwenendo wake ndani ya kikosi hicho, Chilambo amesema kuwa pamoja na kutekeleza majukumu ya ulinzi, mara kwa mara hutumia uwezo wake anapofika eneo la mwisho la kushambulia ili kuongeza nguvu na tija katika kusaka mabao.

Beki huyo aliyesajiliwa akitokea Azam FC, ameeleza kuwa Kocha Barker amempa uhuru mkubwa anapofika eneo la mpinzani, jambo linalomfanya ajisikie huru kama mchezaji namba 10 au kiunoni.

“Kocha amenipa uhuru ninapokuwa katika eneo la mwisho. Nakuwa huru kama mchezaji namba 10 au Clatous Chama. Mchezaji unapopewa uhuru huo, inamaanisha mwalimu amekuamini, hivyo inakulazimu kupambana kusaidia timu,” amesema Chilambo.

Chilambo alionyesha mfano halisi wa mchango wake katika eneo la ushambuliaji alipofunga bao safi kwenye ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya 15 de Agosto katika Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa anathamini sana imani aliyopewa na benchi la ufundi na kwamba hana mpango wa kumwangusha kocha wala kuwaangusha mashabiki wa Simba wanaotamani mafanikio makubwa msimu huu.

Kikosi cha Yanga Leo: Yanga Kushuka Dimbani Sheikh Amri Abeid Kulipa Kisasi dhidi ya TRA United