Mfungaji Bora Ligi Kuu ya Wanawake: Nani Kuweka Rekodi Mpya Msimu Huu?
ACHANA na vita kali ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL) inayotarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake msimu huu; kuna shughuli nyingine pevu kwenye mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora Ligi Kuu ya Wanawake.
Tangu msimu wa 2018/19, rekodi za wafungaji bora zimekuwa zikionyesha mabadiliko makubwa ya kiushindani. Historia inaanzia kwenye mabao 60 yaliyowekwa na Fatuma Mustapha wa JKT Queens, hadi kufikia mabao 20 yaliyompa ufalme Jeanine Mukandayisenga wa Yanga Princess msimu uliopita.
Wakati timu zikianza safari mpya ya kusaka heshima, swali kubwa kwa mashabiki ni: Nani ataibuka na tuzo hii msimu huu, na je, yupo mshambuliaji atakayeweza kurejesha au kuvunja rekodi ya Fatuma?
Rekodi ya Kutisha ya Fatuma Mustapha
Takwimu zinaonyesha kuwa Fatuma Mustapha ndiye anayeshikilia rekodi ya juu zaidi katika orodha ya wafungaji bora wa WPL kwa misimu minane iliyopita. Katika msimu wa 2018/19, alipachika nyavu mara 60 akiwa na JKT Queens—takwimu ambazo hazijawahi kufikiwa tena na mchezaji yeyote hadi leo.
Msimu uliofuata wa 2019/20, Fatuma aliendeleza utawala wake kwa kufunga mabao 33. Bagolwa huyo aliendelea kuthibitisha ubora wake ingawa idadi hiyo ilipungua kwa mabao 27 ikilinganishwa na msimu wake wa kwanza.
Hata hivyo, misimu iliyofuata ilileta sura mpya na ushindani tofauti:
-
2020/21: Aisha Masaka (Yanga Princess) – Mabao 35
-
2021/22: Asha Djafari (Simba Queens) – Mabao 26
Je, Mabao ya Wafungaji Bora Yanapungua?
Misimu ya karibuni imeonyesha kuporomoka kwa idadi ya mabao ya kinara wa ufungaji ikilinganishwa na enzi za Fatuma na Masaka.
-
2022/23: Jentrix Shikangwa (Simba Queens) – Mabao 17
-
2023/24: Aisha Mnunka (Simba Queens) – Mabao 20
-
2024/25: Stumai Abdallah (JKT Queens) – Mabao 28
-
2025/26: Jeanine Mukandayisenga (Yanga Princess) – Mabao 20
Kwa hesabu za misimu minne iliyopita (2022/23 hadi 2025/26), wastani wa mabao ya mfungaji bora ni mabao 21.25 kwa msimu. Hii inamaanisha kuwa mshambuliaji yeyote kakika msimu huu anahitaji kuanzia wastani wa mabao 20 ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa kiatu.
Utawala wa Simba, Yanga na JKT Queens
Takwimu hazidanganyi; vilabu vya JKT Queens, Simba Queens na Yanga Princess vimekuwa kiwanda cha kuzalisha wafungaji bora wa ligi:
-
JKT Queens: Imotoa wafungaji bora kupitia Fatuma Mustapha (mara mbili) na Stumai Abdallah.
-
Simba Queens: Imewahi kutwaa tuzo hiyo kupitia Asha Djafari, Jentrix Shikangwa, na Aisha Mnunka.
-
Yanga Princess: Imewatoa Aisha Masaka na Jeanine Mukandayisenga.
Uwezo wa kutengeneza nafasi na kufunga wa timu hizi unaonekana wazi katika takwimu zao za msimu uliopita, ambapo Yanga Princess ilifunga mabao 56 huku Simba Queens ikipachika mabao 52 kwenye mechi 22.
Kimbunga cha Masajili: Wafungaji Bora Wametimka!
Mbio za msimu huu zinaingia kwenye sura mpya baada ya vinara wa msimu uliopita kuondoka nchini:
-
Jeanine Mukandayisenga (Mfungaji bora 2025/26 – mabao 20) aliondoka Yanga Princess na kujiunga na Wuhan Jiangda ya China mwezi Julai 2026.
-
Jentrix Shikangwa (mabao 16 msimu uliopita) ametimkia FC Masar ya Misri.
Kutokana na kuondoka kwao, meza ipo wazi kwa majina mapya kutengeneza historia yao. Hata hivyo, Stumai Abdallah endapo ataendelea kuitumikia JKT Queens, anabaki kuwa tishio kubwa kurejesha au kuongeza rekodi yake ya mabao 28.
Uso Mpya: Nani Anapewa Nafasi Msimu Huu?
Nyota wapya waliosajiliwa hivi karibuni wanatazamiwa kuleta ushindani mkubwa kwenye mbio za mfungaji bora Ligi Kuu ya Wanawake:
-
Senaf Demise (Simba Queens): Anaingia WPL akiwa na historia ya kutisha kutoka ligi ya Ethiopia na mashindano ya CECAFA. Rekodi yake ya mabao 21 katika mechi 20 (mwaka 2019) na mabao sita ya CECAFA (2024) inamdhihirisha kama mashine ya mabao.
-
Sandrine Mutuyimana (Yanga Princess): Mshambuliaji huyu anajiunga na Yanga akitokea Rwanda ambako aliondoka akiwa kinara wa mabao (mabao 10).
-
Mesay Temsgen (Yanga Princess): Kiungo huyu mshambuliaji raia wa Ethiopia naye ameonyesha viashiria vya kuingia kwenye vita ya kuwania kiatu hiki.
Neno la Mwisho
Rekodi ya mabao 60 ya Fatuma Mustapha inabaki kuwa mlima mrefu kupanda katika historia ya WPL. Hata hivyo, msimu huu macho yote yatakuwa kwa mshambuliaji atakayevuka kizingiti cha mabao 20 na kuweka viwango mpya.
Je, kiatu kitaenda JKT Queens, Simba Queens, au Yanga Princess? Au kuna timu nyingine itakayomtoa mfungaji bora wa kuwashangaza wengi? Majibu yote yatapatikana uwanjani!