Rushine De Reuck Aibuka Shujaa Simba SC: “Pointi 3 Ndicho Kiitu cha Muhimu”
Nahodha wa Simba SC, Rushine De Reuck, amesisitiza kuwa jambo la msingi zaidi kwa sasa ni kupata matokeo mazuri na kukusanya pointi tatu ili kuendeleza mbio zao za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hata kama timu haijafikia kiwango cha juu kinachotarajiwa na mashabiki.
Kauli hiyo ya De Reuck imekuja mara baada ya kuifungia Simba SC bao pekee la ushindi katika mchezo mgumu wa Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate FC, uliopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, na kuibuka shujaa wa mchezo huo.
Akizungumza mara baada ya txu ya mchezo huo, beki huyo wa kati alieleza kufurahishwa kwake na mchango wake katika kuipa timu matokeo, ingawa alikiri wazi kuwa viwango vyao uwanjani havikuridhisha.
“Pointi tatu ni pointi tatu. Nina hisia mchanganyiko; kwa upande mmoja ninafurahi kwa sababu nimeweza kuisaidia timu kushinda, lakini sidhani kama tulicheza mchezo wetu bora leo,” alisema De Reuck.
De Reuck aliongeza kuwa kucheza mechi za ugenini si kazi rahisi, hususan pale timu inapokabiliwa na ratiba mbana ya kucheza kila baada ya siku tatu, hali inayowataka wachezaji kuwa na utulivu, nguvu pamoja na kujituma kwa kiwango cha juu.
Pamoja na kutoridhishwa na kiwango cha uchezaji, nahodha huyo alipongeza jitihada na roho ya kupambana iliyoonyeshwa na wachezaji wenzake, akisisitiza haja ya kujenga utamaduni wa kushinda mechi bila kujali changamoto za mazingira.
“Najivunia juhudi za wachezaji wenzangu. Haikuwa rahisi kucheza ugenini, hasa tunapocheza kila baada ya siku tatu. Wachezaji wameonyesha tena moyo mkubwa wa kupambana na ni muhimu kujenga utamaduni wa kushinda. Tunachopaswa kufanya ni kuendelea kushinda,” aliongeza.
Ushindi huo unaendelea kuipa Simba SC kasi nzuri katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, huku Rushine De Reuck akizidi kudhihirisha umuhimu wake kikosini kwa kuimarisha safu ya ulinzi na kufunga mabao muhimu.