Yanga SC Ligi ya Mabingwa Afrika
Yanga SC

Kamwe Atoa Tamko Zito Ligi ya Mabingwa: “Tutabonda Nyumbani, Kunyonga Nje!”

Vardo November 3, 2026 9:59 am

Msemaji wa Yanga SC, Ali Kamwe, amerejesha matumaini makubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo kuelekea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026/27, akisisitiza kuwa hakuna mpinzani katika Kundi B mwenye uwezo wa kuwatisha au kuzuia ndoto zao.

Yanga imepangwa katika Kundi B ambalo linatajwa kuwa miongoni mwa makundi magumu, likizikutanisha timu zenye historia kubwa barani Afrika—Zamalek ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain ya Tunisia. Licha ya timu tatu kati ya hizo kutokea Kaskazini mwa Afrika, Kamwe ameweka wazi kuwa Yanga haina sababu ya kuwaogopa wapinzani wao.

Malengo ni Robo Finali

Akizungumza kuhusu malengo ya klabu hiyo, Kamwe ameeleza kuwa shabaha kuu ni kumaliza katika nafasi mbili za juu ili kufuzu hatua ya robo fainali bila mashaka yoyote.

“Wapinzani wetu hawana chochote cha kututisha. Lengo letu ni moja tu—kuvuka hatua ya makundi na kusonga mbele hadi robo fainali. Kundi hili si gumu, na kama kutakuwa na ugumu wowote basi tutakuwa tumejiletea wenyewe,” amesisitiza Kamwe.

Licha ya wapinzani wao kutwaa ubingwa wa ligi zao za ndani msimu uliopita, Kamwe amekumbusha kuwa Yanga nayo ina heshima kubwa baada ya kutwaa ubingwa wa Tanzania. Aidha, ametaja nafasi ya tano inayoshikiliwa na Ligi ya Tanzania katika ubora wa ligi za Afrika kama chachu na sababu ya msingi ya wao kujiamini.

Kaulimbiu Mpya: Kubonda Nyumbani, Kunyonga Nje

Kamwe amebainisha kuwa benchi la ufundi linafanyia kazi mapungufu yote ya kiufundi yaliyojitokeza kwenye mechi za hivi karibuni ili kuingia kwenye ushindani wakiwa imara 100%.

“Naamini tukirekebisha baadhi ya mambo yetu ya kiufundi yaliyokuwa changamoto, kaulimbiu tuliyoingia nayo ya kubonda na kunyonga itaonekana kwa vitendo. Tutabonda watu hapa Tanzania na kwenda kuwanyonga huko huko kwao. Hatuna mashaka na hilo.”

Imani Kubwa kwa Benchi Jipya la Ufundi

Katika hatua nyingine, msemaji huyo ameonyesha kuamini zaidi benchi jipya la ufundi la Yanga, akieleza kuwa lina uzoefu na uelewa wa kutosha kuhusu soka la Kaskazini mwa Afrika pamoja na mazingira ya nchi za timu pinzani.

Amehitimisha kwa kusema kuwa morali ya wachezaji iko juu sana na hiyo ndiyo spirit inayotakiwa kuelekea mechi za hatua hiyo.

Kampeni za Yanga SC katika hatua ya makundi zinatarajiwa kuanza rasmi kati ya Novemba 27 na 29 mwaka huu, ambapo wataanza kusaka pointi muhimu zitakazowavusha kwenda robo fainali.

Steve Barker Aweka Historia Simba SC: Ushindi wa Mechi 20 Mfululizo Ligi Kuu! Yanga SC Kusubiri Kocha Mpya Kupanga Programu ya Mapumziko ya FIFA