Kocha Mpya Yanga SC
Yanga SC

Kocha Mpya Yanga SC Kutambulishwa Siku 2 Zijazo | Mabadiliko Makubwa Benchi la Ufundi

Vardo November 3, 2026 10:08 am

Uongozi wa klabu ya Yanga SC umewatoa hofu wanachama na mashabiki wake baada ya kutangaza kuwa mchakato wa kumpata kocha mpya wa timu hiyo umekamilika rasmi, na anatarajiwa kutambulishwa ndani ya siku mbili zijazo mara baada ya kukamilika kwa taratibu za mwisho.

Mabadiliko haya yanakuja baada ya uongozi kufanya tathmini ya kina ili kumpata mwalimu atakayeweza kukabiliana na ushindani wa msimu huu katika mashindano mbalimbali, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC Premier League), na Kombe la CRDB Federation Cup.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Msemaji wa Yanga SC, Ali Kamwe, ameeleza kuwa kwa sasa klabu ipo katika hatua za mwisho za kuweka sawa benchi jipya la ufundi kulingana na matakwa ya kocha huyo mpya.

“Naweza kuwathibitishia wanachama na mashabiki wa Yanga kwamba tayari mchakato umekamilika. Kumekuwa na mabadiliko kwenye benchi la ufundi kwa sababu kocha mpya ana matakwa yake ya watu anaotaka kufanya nao kazi, na sisi tunafanya mazungumzo kuhakikisha tunajenga benchi imara,” alisema Ali Kamwe.

Mabadiliko Makubwa Benchi la Ufundi

Ali Kamwe aliongeza kuwa lengo kuu la uongozi ni kuhakikisha timu inapata benchi la ufundi lenye wataalamu wa kutosha katika kila idara ili kukidhi matarajio makubwa ya mashabiki na malengo ya klabu kimataifa na ndani ya nchi.

Pia Atapewa Muda wa Kuandaa Programu Zake

Kocha huyo mpya atapewa nafasi na muda wa kutosha wa kuandaa programu zake za mafunzo kabla ya kuanza rasmi majukumu ya kuifundisha timu hiyo uwanjani.

“Ndani ya siku mbili hizi, Insha Allah, tutamtambulisha kocha mpya. Tumempa muda wa kupanga programu zake vizuri kwa sababu tukisham tangaza tu, kazi ya kuiandaa timu kwa ajili ya michezo inayofuata ya Ligi Kuu na Klabu Bingwa inaanza mara moja,” alihitimisha Kamwe.

Hatua hii inaashiria mwanzo wa ukurasa mpya ndani ya kikosi cha Wananchi, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona ni nani atachukua mikoba ya kuongoza jahazi hilo kuelekea mafanikio ya msimu huu.

Yanga SC Kusubiri Kocha Mpya Kupanga Programu ya Mapumziko ya FIFA Steve Barker Asifu Roho ya Kupambana Simba SC Dhidi ya Namungo FC