Steve Barker Kutumia Mapumziko ya FIFA Kuisuka Upya Simba SC
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, anatarajiwa kutumia kikamilifu kipindi hiki cha mapumziko ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kufanya tathmini ya kina ya kikosi chake ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kurejea kwa michezo ya ushindani.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameeleza kuwa mapumziko hayo yatatoa fursa nzuri kwa Barker na benchi lake la ufundi kupitia michezo iliyopita, kubaini maeneo yaliyofanya vizuri pamoja na yale yanayohitaji kufanyiwa kazi mara moja.
Ahmed amesisitiza kuwa tathmini hiyo ni nguzo muhimu katika kuimarisha kiwango cha timu, kwani itaiwezesha benchi la ufundi kufanya marekebisho ya kiufundi na kuweka mikakati thabiti itakayohakikisha Simba inaendelea kuwa katika hali ya ushindani wa juu.
Aidha, klabu hiyo inaona ni muhimu kutumia vyema mapumziko haya kujiandaa na kalenda nzito inayowakabili mbele yao, hasa ikizingatiwa kuwa Simba inakabiliwa na kibarua kizito cha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wapinzani wenye uzoefu na ushindani mkubwa.
Kuhusu mipango ya kambi na michezo ya kirafiki, Ahmed amebainisha kuwa kwa sasa bado hakuna taarifa rasmi. Hata hivyo, mara baada ya taratibu zote kukamilika, uongozi wa klabu utatoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari na mashabiki ili kuwajulisha utaratibu kamili wa maandalizi hayo.
Wachezaji wa Simba wataendelea kuwa mapumzikoni hadi Novemba 9, ambapo watarejea kikosini kuanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kinyang’anyiro cha Ligi ya Mabingwa Afrika.