Ben White England
Meridianbet

Ben White Afunguka: Sababu za Kugoma England na Ukweli Kuhusu Kombe la Dunia Qatar

Vardo November 10, 2026 4:03 pm

LONDON, ENGLAND – Beki kisiki wa Arsenal, Ben White, ameweka wazi kuwa mashabiki wa timu ya taifa ya England (Three Lions) wangeacha kumzomea kama tu wangefahamu picha kamili na ukweli wote uliojificha nyuma ya uamuzi wake wa kuondoka kambini ghafla wakati wa Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

White, ambaye alitema kambi hiyo baada ya hatua ya makundi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni “sababu binafsi”, hatimaye amefunguka kwa kina kuhusu sakata hilo ambalo limekuwa mwiba mkali na kumuweka chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wa nchi hiyo. Katika kipindi hicho, minong’ono ilisema kulikuwa na mgogoro mzito kati yake na msaidizi wa kocha wa wakati huo, Gareth Southgate, yaani Steve Holland.

Baada ya tukio hilo, White aligoma kurejea kikosini kwa muda wote ambao Southgate na Holland waliendelea kuinoa timu hiyo. Hata hivyo, hali ilibadilika alipoteuliwa tena na kocha mpya, Thomas Tuchel, mwezi Machi mwaka huu.

Licha ya kurejea kwake, mapokezi hayakuwa ya maua. Alipokelewa kwa kuzomewa vikali na mashabiki wa England aliporudi uwanjani Wembley kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Uruguay. Hata hivyo, beki huyo mwenye umri wa miaka 29 alijibu kwa vitendo—akifunga bao lake la kwanza la taifa kabla ya kusababisha penalti ya dakika za mwisho katika mchezo uliomalizika kwa sare ya 1-1.

“Siwezi kumtupia mtu lawama”

Akizungumzia kwa mara ya kwanza hisia zake kuhusu kuzomewa na umati uliokuwa ukimshangilia hapo awali, White alikiri haikuwa rahisi kumeza hali hiyo:

“Haikuwa rahisi kusikia wakinizomea, hasa kwa sababu hawakujua hali halisi iliyokuwepo. Watu hawajui mazingira yangu wala sababu zilizoniumba nifanye hivyo. Kama wangejua, naamini kabisa wasingenizomea wala kusema mambo yale.”

Aliongeza kuwa pamoja na kuona kila aina ya taarifa na uvumi uliotapakaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, hana mpango wa kumuanika mtu au kuanika siri zote zilizojiri ili kujisafisha:

“Kuna mengi yamesemwa na nimeona takriban kila kitu kilichoandikwa. Lakini sitaki kumtupia mtu lawama au kumuweka mtu kwenye wakati mgumu. Kulikuwa na changamoto za mawasiliano, lakini ninafurahi kuwa hapa sasa na ni heshima kubwa kuitwa tena kuitumikia nchi yangu.”

Kwa sasa, Ben White yuko tayari na ananoa makali yake kuelekea michezo ijayo ya Ligi ya Mataifa dhidi ya Croatia na Hispania, huku akiwa na matumaini kwamba ukurasa mpya utawafanya mashabiki wamtazame kwa jicho tofauti.

Gates Of Meridian Yaingia Uwanjani, Meridianbet Yaleta Burudani Mpya Kutoka Expanse Declan Rice Afunguka Aina ya Maisha Anayomlea Mwanaye, Aacha Mitandao