Declan Rice mitandao ya kijamii
Habari za michezo

Declan Rice Afunguka Aina ya Maisha Anayomlea Mwanaye, Aacha Mitandao

Vardo November 10, 2026 4:15 pm

LONDON, ENGLAND – Kiungo mahiri wa Arsenal na timu ya taifa ya England, Declan Rice, amefunguka wazi kuhusu uamuzi wake wa kupunguza matumizi ya mitandao ya kijamii, akibainisha kuwa taarifa na maoni hasi kwenye majukwaa hayo yana uwezo wa kumharibia mtu siku nzima.

Rice (27), ambaye amekuwa muhali wa ukosoaji na mashambulizi ya mtandaoni kutoka kwa baadhi ya mashabiki, ameeleza kuwa amejifunza mbinu ya kujitenga na kelele zisizo na manufaa ili kulinda utulivu wa akili yake.

Nyota huyo aliyefanya mahojiano maalum na jarida mashuhuri la GQ baada ya kutajwa miongoni mwa watu mashuhuri wa mwaka, alibainisha kuwa alifuta kabisa matumizi ya mtandao wa X (zamani Twitter) miaka mitatu iliyopita.

“Bado sijarudi tena kwenye mtandao huo. Unaweza kuamka asubuhi ukiwa na furaha tele, lakini ukasoma ujumbe mmoja tu mbaya na ghafla siku yako nzima ikaharibika,” alisema Rice.

Shambulio la Mtandaoni Kwaye na Mwenza Wake

Uamuzi wa Rice unakuja kufuatia matukio ya nyuma ambapo mwenza wake wa muda mrefu, Lauren Fryer, alilengwa na mashambulizi ya kejeli kuhusu muonekano wake, hali iliyomfanya Fryer kufuta picha na machapisho yake yote kwenye mtandao wa Instagram mwaka 2024.

Rice, ambaye amebarikiwa kupata mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne (Jude) akiwa na Fryer, alieleza kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto wadogo ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa katika ulimwengu wa sasa.

“Kwangu mimi muda ninaotumia kwenye simu si tatizo. Lakini ninaamini mitandao ya kijamii kwa watoto ni janga kwa asilimia 100. Sioni tena ule upekee wa tabia na haiba ya asili tuliyokuwa nayo miaka michache iliyopita,” aliongeza.

Mkataba Mpya Arsenal na Malezi ya Mtoto

Nje ya uwanja, Rice anakaribia kusaini mkataba mpya wa muda mrefu na klabu ya Arsenal ambao utamwezesha kuvuta mshahara wa takribani Pauni 350,000 (Shilingi Bilioni 1.2 za Kitanzania) kwa wiki. Mkataba huo utamweka kileleni mwa wachezaji wanaolipwa fedha nyingi zaidi klabuni hapo sambamba na Bukayo Saka.

Pamoja na mafanikio na utajiri huo mkubwa, Rice amesisitiza umuhimu wa kumfundisha mwanaye thamani halisi ya maisha na fedha badala ya kumdekeza.

“Fedha zinazozunguka kwenye soka ni nyingi sana. Ni muhimu mtoto aelewe gharama za vitu hata kama huna wasiwasi wa kuvilipia. Unataka ajifunze kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu wakubwa na wadogo, na kuelewa jinsi dunia inavyokwenda,” alimalizia kiungo huyo.

Kwa sasa, Declan Rice anaendelea kuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Arsenal kinachowania mataji mbalimbali msimu huu.

Ben White Afunguka: Sababu za Kugoma England na Ukweli Kuhusu Kombe la Dunia Qatar Xabi Alonso Aanza Kupitia Wakati Mgumu Chelsea: Mashabiki Waanza Kupoteza Imani