Namungo FC na Geita Gold Vitani Kumgombea Ladack Chasambi
Klabu ya Namungo FC imeingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha kuwania saini ya kiungo mshambuliaji hatari, Ladack Chasambi, ambaye pia anawindwa kwa ukaribu na maafande wa Geita Gold, huku kocha mkuu wa kikosi hicho, Juma Mgunda, akitajwa kuwa karata muhimu ya kufanikisha usajili huo.
Chasambi, nyota wa zamani wa Mtibwa Sugar na Simba SC, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na Singida Black Stars hivi karibuni, hali inayozifanya klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara kupigana vikumbo kupata huduma yake.
Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo vimeeleza kuwa benchi la ufundi la Namungo limepanga kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kumsajili winga huyo kijana mwenye kasi, chenga za maudhi, na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao. Jina la Chasambi limepewa kipaumbele cha juu na Kocha Mgunda.
“Kocha anaamini Ladack Chasambi anaweza kuongeza ushindani mkubwa kwenye kikosi chake. Ndiyo maana uongozi umeingia vitani kumshawishi asaini, ingawa tutalazimika kupambana na upinzani mkali kutoka Geita Gold ambao nao wanamhitaji,” kilieleza chanzo hicho.
Turufu ya Juma Mgunda Katika vita hii ya usajili, Namungo FC inaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi kutokana na uwepo wa Kocha Juma Mgunda. Wawili hao waliwahi kufanya kazi pamoja wakiwa Simba SC, jambo linalompa Mgunda uelewa mpana wa kipaji, nidhamu, na namna bora ya kumtumia kiungo huyo uwanjani.
Kwa sasa, Namungo FC inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ikiwa imekusanya pointi 15 baada ya kushuka dimbani mara 11, na inalenga kufanya maboresho makubwa ili kumaliza katika nafasi za juu msimu huu.