Bruno Fernandes Manchester United
Habari za michezo

Bruno Fernandes Afunguka Hatima Yake Manchester United na Mkataba Mpya

Vardo November 22, 2026 2:56 pm

NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes, amevunja ukimya kuhusu mustakabali wake ndani ya klabu hiyo, akithibitisha kuwa amepokea ofa ya mkataba mpya lakini ameamua kusitisha mazungumzo hayo kwa muda.

Kiungo huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 32 anatarajiwa kumaliza mkataba wake wa sasa mwishoni mwa msimu huu, ingawa mabingwa hao wa kihistoria wa England wana kipengele kinachowaruhusu kuongeza mwaka mmoja zaidi hadi mwaka 2028.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Sky Sports, Fernandes alisema hatua ya uongozi wa Manchester United kumpa ofa mpya ni ishara tosha kuwa bado wanahitaji huduma yake katika dimba la Old Trafford. Hata hivyo, alikanusha vikali tetesi kuwa anashinikiza kuongezewa mshahara mkubwa.

“Klabu imetoa ofa ya mkataba mpya, hivyo nadhani hilo linaonyesha kuwa kwa upande wao wanataka nibaki. Kwa sasa hakuna mazungumzo yanayoendelea, lakini nimeona watu wakisema nimeomba mshahara mkubwa zaidi au miaka mingi zaidi. Kama ningekuwa nataka fedha nyingi zaidi, nisingekuwa hapa,” alisema Fernandes.

Alikataa Ofa Nono Ili Kubaki Old Trafford

Fernandes aliongeza kuwa katika misimu michache iliyopita alipata fursa za kuondoka Manchester United na kujiunga na klabu nyingine zilizokuwa tayari kumpa maslahi makubwa ya kifedha, lakini mapenzi yake kwa timu hiyo yalimfanya abaki.

“Nilikuwa na sehemu ambayo ningeweza kwenda na kupata fedha nyingi zaidi kuliko ninazopata hapa, na hata kwenda sehemu yenye hali ya hewa ya joto zaidi kuliko Manchester. Miaka miwili, mitatu iliyopita na hata majira ya kiangazi yaliyopita nilikuwa na nafasi ya kuondoka, lakini kila mara nilichagua kubaki,” alisisitiza.

Kauli hii inakuja siku chache baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo, Omar Berrada, kudokeza kuwa walikuwa kwenye mazungumzo ya siri kuhusu mkataba wa nahodha huyo.

Sababu ya Kusitisha Mazungumzo ya Mkataba

Tangu alipojiunga na Manchester United akitokea Sporting CP mwaka 2020, Bruno Fernandes amefunga mabao 75 katika Ligi Kuu England na kuweka rekodi ya asisti nyingi ndani ya msimu mmoja msimu uliopita.

Licha ya mafanikio hayo binafsi, mwanzo mbaya wa timu msimu huu—ambao uliwashuhudia wakishuka hadi nafasi ya 19 kwenye msimamo kabla ya kibarua cha kocha mpya Mauricio Pochettino dhidi ya Liverpool—umemfanya aone si busara kujadili maslahi binafsi.

“Tulianza kuzungumza mwishoni mwa msimu uliopita na tuliporejea mwanzoni mwa msimu huu tukajadili tena. Lakini kwa kuzingatia hali ya timu kwa sasa, niliamua kuliweka pembeni suala hili. Jambo muhimu zaidi kwa sasa ni klabu kurejea kwenye ushindi,” alifafanua.

Ukweli Kuhusu Madai ya Mgogoro na Michael Carrick

Katika hatua nyingine, nahodha huyo amekanusha taarifa zilizokuwa zikidai kuwa aliingia kwenye mgogoro na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Michael Carrick, ambaye alifutwa kazi Novemba 12.

Tetesi hizo ziliibuka baada ya Fernandes kuachwa benchi kwenye mchezo dhidi ya Bournemouth mwezi uliopita, siku chache baada ya kukosoa mbinu za timu kufuatia kipigo kizito dhidi ya Como katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Fernandes ameeleza kuwa Carrick alimfuata binafsi na kumweleza kuwa uamuzi huo ulikuwa wa kiufundi tu:

“Kocha alikuja kuzungumza nami kabla ya mechi dhidi ya Bournemouth na kuniambia: ‘Sikuanzi na wewe kesho. Hilo halihusiani na maneno yako kuhusu Como, najua watu watajaribu kulihusisha na hilo. Lazima nifanye mabadiliko kwa sababu kiwango cha timu hakijakuwa kizuri.’”

Simba vs Orlando Pirates Novemba 29: Ahmed Ally Afunguka Kipimo cha JKT Tanzania! Pigo Zito Bayern Munich: Jeraha la Harry Kane Lamweka Nje Miezi 4!