Singida Black Stars vs AS Maniema Union
Michezo Bongo

Kimoto Afichua Siri ya Mchana Kuimaliza AS Maniema Union

Vardo November 25, 2026 12:00 pm

Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Papy Kimoto, ameanza rasmi operesheni ya kuhakikisha kikosi chake kinaibuka na ushindi ugenini dhidi ya AS Maniema Union ya DR Congo, katika mchezo wa ufunguzi wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika kuhakikisha mbinu zake zinafanikiwa, Kimoto amepanga kutumia siku tano mfululizo kufanya mazoezi ya jua kali la mchana jijini Dar es Salaam, kabla ya kikosi hicho kuanza safari ya kuelekea DR Congo Novemba 27.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Kimoto alifafanua kuwa uamuzi wa kubadili muda wa mazoezi umetokana na tathmini ya kina ya hali ya hewa nchini DR Congo, ambayo kwa sasa ina joto kali linaloshabihiana na lile la Dar es Salaam. Lengo kuu ni kuwafanya wachezaji wake kuzoea mazingira hayo mapema kabla ya kushuka dimbani.

Mtihani wa Hisia Dhidi ya Waajiri Wake wa Zamani

Mchezo huu wa Singida Black Stars vs AS Maniema Union unabeba hisia za kipekee kwa kocha huyo, kwani anakwenda kukutana na timu aliyoijenga kwa mikono yake kwa takribani miaka minne tangu Januari 2022.

“Hapa na Congo hali ya hewa ni ya jua, ni sawa. Tumefanya tathmini, msimu huu ni mgumu kwenye michuano ya kimataifa na nimeifundisha Maniema. Ni furaha kwangu kukutana na timu niliyowahi kuifundisha na msimu uliopita ilifika robo fainali,” alisema Kimoto.

Rekodi ya Kimoto Akiwa na AS Maniema Union

Kimoto anaingia kwenye mchezo huu akiifahamu fika Maniema Union kutokana na mafanikio makubwa aliyowapa:

  • Ligi ya Mabingwa Afrika (2024/25): Aliweka historia ya kuipeleka klabu hiyo hatua ya makundi kwa mara ya kwanza, ikipangwa kundi gumu na vigogo Mamelodi Sundowns, Raja Casablanca na AS FAR, ambapo ilimaliza na pointi tatu.

  • Kombe la Shirikisho Afrika (Msimu Uliopita): Aliiongoza kufika hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi B ikiwa na pointi 12, nyuma ya Wydad Casablanca iliyokusanya pointi 15.

Kurekebisha Makosa ya Mwanzo wa Msimu

Pamoja na matumaini makubwa aliyonayo, Kimoto hakusita kukiri kuwa Singida Black Stars haikuwa na mwanzo mzuri wa msimu kutokana na maandalizi duni ya awali (pre-season) pamoja na usajili ambao haukukidhi mahitaji ya haraka, hali iliyosababisha matokeo ya kupanda na kushuka.

“Tunapaswa kutengeneza timu vizuri kwa sababu mwanzoni tulifanya makosa mengi. Pre-season yetu haikuwa nzuri na usajili haukuwa mzuri. Hata hivyo, tumesharekebisha eneo la utimamu wa mwili (fiziki) na sasa tunapambana kuimarisha maeneo mengine,” alisisitiza kocha huyo.

Aliongeza kuwa changamoto ya kutowafahamu wachezaji wake kwa undani ilimfanya abadilidilishe kikosi mara kwa mara, lakini sasa anatumia programu ya mazoezi ya siku hizi tano kutathmini uwezo wa kila mchezaji na nafasi sahihi anayoweza kuitumikia ili kuishangaza AS Maniema Union ugenini.

Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya Leo: Takwimu, Utabiri na Vikosi Tanzia Nollywood: Mwigizaji Mkongwe Pete Edochie Afariki Dunia Akiwa na Miaka 79