Home Uncategorized ZIDANE ANA MAMBO MANNE YA KUWEKA SAWA REAL

ZIDANE ANA MAMBO MANNE YA KUWEKA SAWA REAL


BAADA ya kufanya vibaya msimu huu wa 2018/19, uongozi wa Real Madrid unakabiliwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri msimu ujao.

Real Madrid imekamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga ikiwa na pointi 19 nyuma ya wapinzani wao wa jadi, Barcelona, ambao wamenyakua ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.

Kibaya zaidi ilitolewa kwenye hatua ya mtoano wa 16 bora na Ajax Amsterdam. Real Madrid ina rekodi mbovu katika La Liga katika misimu ya karibuni ikiwa imetwaa ubingwa mara moja wa La Liga katika misimu saba.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane ana kibarua cha kufanya mambo manne ili kuweza kurudisha makali ya timu hiyo, ambayo inashikilia rekodi ya kutwaa mara nyingi zaidi ubingwa wa La Liga na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

AMTUMIE ZAIDI VINICIUS

Vinicius Jr bado ana umri wa miaka 18 lakini katika mechi ambazo amechezeshwa ameonyesha kuwa ni moto. Atakuwa silaha ya maana ya kuongeza makali ya Real Madrid kutokana na mabeki wengi kushindwa kwenda na kasi na chenga zake. Zidane anapaswa kumsaidia Vinicius aweze kufunga mabao mengi zaidi kutokana na ukweli kuwa rekodi yake ya kufunga mabao bado sio nzuri. Tangu ameanza kujumuishwa kikosi cha wakubwa cha Real Madrid msimu wa 2018/19, amecheza mechi 31 na kupachika mabao manne.

KASI NDOGO YA MASHAMBULIZI REAL

Real Madrid inakabiliwa na tatizo la kushindwa kushambulia kwa kasi timu pinzani. Tatizo hili limejitokeza katika nyakati tofauti wakati timu ikinolewa na Julen Lopetegui, Santiago Solari na sasa Zidane. Nyota wa kutengeneza mashambulizi wa Real Madrid kama Marcelo, Toni Kroos na Isco kwa sasa wanaonekana kupungua uwezo.

Kuna mechi nyingi tu ambazo Real Madrid ilishindwa kasi na timu pinzani kama ilivyotokea kwenye mechi kadhaa msimu huu kwa mfano dhidi ya Ajax, Eibar, Huesca, Sevilla, Athletic Bilbao, Rayo Vallecano na nyingine nyingi. Zidane atapaswa kuja na maarifa mapya ya namna ya kutengeneza mashambulizi ya Real Madrid ukizingatia timu hii haina tena Cristiano Ronaldo, ambaye alikuwa tishIo kwa timu pinzani.

TATIZO LA MARCELO

Beki wa kushoto, Marcelo alikuwa anahusika kwa kiasi kikubwa kutengeneza mashambulizi ya Real Madrid. Msimu huu mara kadhaa Marcelo amekuwa anawekwa benchi na nafasi yake kuchukuliwa na kinda Sergio Reguilon. Marcelo alikuwa ni mzuri wa krosi na pasi za mabao lakini inaonekana wazi kuwa makali yake yameanza kupungua. Hata hivyo, Zidane amesisitiza kuwa ataendelea kumtumia Marcelo na beki wake wa kushoto.

MUSTAKABALI WA YOSSO

Zidane atakuwa na mtihani wa kukuna kichwa wa namna ya kuwatumia yosso kama Vincius Jr, Reguilon na Marcos Llorente. Wachezaji hawa katika nafasi chache walizopewa msimu huu walionyesha uwezo mkubwa. Vinicius alikuwa moto katika kutengeneza mashambulizi huku Reguilon akifanya kazi ya kuziba pengo la Marcelo alipopewa nafasi kama beki wa kushoto. Llorente naye amekuwa anafanya vizuri pale alipokuwa anapewa nafasi kwenye sehemu ya kiungo.

SOMA NA HII  A-Z KUHUSU ISHU YA KAKOLANYA SIMBA IPO NAMNA HIVI