Home Uncategorized SIRI IMEVUJA DIMPOZ, ZARI WALALA NYUMBA YA MONDI

SIRI IMEVUJA DIMPOZ, ZARI WALALA NYUMBA YA MONDI


ACHANA na mapichapicha ya Nairobi nchini Kenya yaliyosambaa kama moto wa kifuu kwenye mitandao ya kijamii, taarifa mpya imevuja kwamba, msanii wa Bongo Fleva, Omar Faraj Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ na mrembo wa Kiganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ wamelala katika ile nyumba ya Sauz ambayo Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alimpa mrembo huyo aliyezaa naye watoto wawili, twende taratibu! 

Diamond au Mondi ambaye ni mkali wa Bongo Fleva, alimpa Zari nyumba hiyo miaka kadhaa iliyopita wakati wakiwa kwenye penzi motomoto kabla ya wawili hao kumwagana mazima.

TUPATE HABARI KAMILI

Chanzo makini kilicho karibu na Dimpoz kimenyetisha kuwa, licha ya mapichapicha hayo yaliyosambaa kuanzia Jumapili iliyopita mitandaoni, wawili hao walipata pia fursa ya kwenda kujiachia katika nyumba hiyo ya Mondi kwa nyakati tofauti.

“Iko hivi Dimpoz na Zari mbona washalala huko nyuma na hata juzi baada ya kusambaa haya mapichapicha ya Kenya mliyoyaona, walikwenda Sauz pamoja na wakalala tena katika ile nyumba ya Diamond,” kilisema chanzo hicho.

NI WAPENZI?

Chanzo hicho kilieleza kuwa, wawili hao ni wapenzi japo wenyewe hawajaamua kuweka wazi na mara nyingi hupenda kutoa picha zao bila maelezo na hata wanapohojiwa husingizia kuwa kuna ‘project’ wanafanya lakini hata hivyo haijawahi kuonekana project yao yoyote ya pamoja.



“Husingizia tu project lakini lini wewe umewahi kusikia project ya Zari na Dimpoz? Hawa ni wapenzi sema tu ndio hivyo hawajaamua kuutangazia umma kama wanatoka,” kilisema chanzo hicho.SIO SIRI TENA!

Aidha, chanzo kingine kilichozungumza na Risasi Mchanganyiko moja kwa moja kutoka Sauz, kimeeleza kuwa, kwa kule penzi lao sio siri tena kwani huwa wakifika wanajiachia kama mtu na mtuwe kabisa. Kilisema kuwa, mbali na picha zilizosambaa zipo nyingine za muda kidogo ambazo zilisambaa baada tu ya Dimpoz kutoka hospitali alipokuwa ameugua kwa muda mrefu.

“Si unakumbuka kuna picha fulani zilivuja kipindi kile Dimpoz ametoka kuumwa, basi tangu hapo walikuwa tayari ni wapenzi lakini wakawa hawaonekani mara kwa mara kwa sababu ya kila mtu kuwa bize na shughuli zake,” kilieleza chanzo hicho.

ATAMUOA?

Risasi Mchanganyiko lilikirudia tena chanzo kilicho karibu na Dimpoz anayekimbiza na Wimbo wa One & Only ambapo kilipopatikana kiliweza kusherehesha ubuyu huu kwa kusema jamaa yuko tayari kwa lolote.

“Kwa jinsi nilivyoona jamaa amezimika hivyo anaweza hata kumuoa maana si unajua tena dada yetu hana tatizo yeye ukimuambia kuzaa anazaa tu, ukimwambia ndoa pia anakubali tu maana ndio kwanza anazidi kuwa binti badala ya kuzeeka,” kilisema chanzo hicho.

DIMPOZ ANASEMAJE?

Baada ya kuupata ubuyu huo wa motomoto, bila kupoteza muda Risasi Mchanganyiko liliamua kumvutia waya Dimpoz kwa njia ya WhatsApp ambapo alipopatikana hakutaka kukubali au kukutaa kama tayari ameingia mazima katika himaya ya penzi la mama wa watoto watano, Zari The Boss Lady. “Ukifika muda wa kulizungumzia hilo kwa undani nitafanya hivyo ila kwa sasa acha tu ibaki kuwa hivyo ilivyo,” alisema Dimpoz.

ZARI ANAMFAA

Alipobanwa zaidi kuhusu ishu ya yeye kulala Sauz mara kadhaa kama ubuyu ulivyotua gazetini, Dimpoz alizidi kusisitiza kuwa muda ukifika atazungumza huku akisema kuwa hakuna ubaya kwani Zari ni mwanamke mzuri na anafaa kumuoa.

“Wewe subiri usiwe na presha muda sahihi ukifika nitaeleza tu ukweli wote. Usiwe na haja ya kunichimbachimba mara hiki mara kile, uzuri ni kwamba Zari ni mwanamke mzuri na anafaa kuolewa na mtu kama mimi,” alisema Dimpoz.

Risasi Mchanganyiko lilizidi kwenda mbali zaidi na kumuuliza kwamba haoni kwa haya mapichapicha yanayosambaa mtandaoni yanaweza kumsababishia uhasama na aliyekuwa mpenzi wa Zari, Diamond Platnumz ambapo hakujibu swali hilo zaidi ya kuishia kucheka kisha kukata simu. Hata alipopigiwa tena, simu iliita kwa muda mrefu bila ya kupokelewa huku Zari simu naye simu yake ikiita muda mrefu bila kupokelewa.

HISTORIA YA DIMPOZ NA MONDI

Miaka kadhaa iliyopita, Dimpoz na Mondi walijikuta kwenye bifu kali kiasi cha kutoleana maneno makali kwa kile kilichodaiwa ni kitendo cha Dimpoz kudaiwa kumnyapia aliyekuwa mpenzi wa Mondi, mrembo Wema Sepetu.

Bifu hilo liliyeyukia hewani na hatukuwahi kusikia wanazungumzia kumaliza tofauti zao na mara kadhaa wamekuwa wakichengachenga kuzungumzia ‘ugomvi’ wao.

Zari mrembo wa Kiganda anayeishi Sauz, ni mama wa watoto watano. Watatu alizaa na marehemu mumewe Ivan Semwanga na wengine wawili amezaa na Mondi ambaye sasa hivi ana kifaa kipya kutoka Kenya, Tanasha Donna.

SOMA NA HII  YANGA WAAENDELEA KUIVUTIA KASI RAYON SPORTS