SIMBA SC WAMVIZIA KIUNGO NYOTA WA STELLENBOSCH FC
Klabu ya Simba SC inatajwa kuwa imeweka mpango maalum wa kuimarisha kikosi chake katika dirisha lijalo la usajili, ambapo sasa macho yao yameelekezwa nchini Afrika Kusini kwa kiungo wa kati wa Stellenbosch FC, Genino Palace.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya klabu hiyo ya Msimbazi, Simba SC imeonyesha dhamira ya kuongeza nguvu katika eneo la kiungo, ikiwa inamfuatilia kwa karibu Palace ambaye anasifika kwa uwezo wake wa kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji kwa ustadi mkubwa.
Inadaiwa kuwa kiungo huyo ana uwezo wa kupandisha na kushusha kasi ya mchezo, huku pia akionekana kuwa na uimara mkubwa wa kiufundi unaomwezesha kudhibiti presha katika mechi zenye ushindani mkubwa.
Chanzo cha karibu na uongozi wa Simba SC kimeeleza kuwa uwepo wa kocha Steven Barker unaweza kuwa moja ya vitu vitakavyorahisisha dili hilo, kutokana na historia yake ya kufanya kazi na mchezaji huyo wakati wote wakiwa ndani ya mfumo mmoja wa Stellenbosch FC.
Kwa upande wake, Palace anaonekana kama mbadala anayelengwa kuchukua nafasi ya kiungo Allasane Kante, ambaye alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu lakini ameshindwa kutoa mchango uliotarajiwa kulingana na mipango ya benchi la ufundi.
Uongozi wa Simba SC unaendelea kusuka mikakati ya kuboresha kikosi chake kwa umakini mkubwa, ukiweka malengo ya kushindania mataji ya ndani na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa msimu ujao.