WPL ILIVYOONDOKA NA UTAMU, MACHUNGU
MSIMU wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL) 2025/26 umetamatika huku Simba Queens ikitwaa taji hilo na kuacha simulizi nyingi zilizoacha alama kwa mashabiki wa soka hilo nchini.
Kulikuwa na vita ya ubingwa, nyota waliotarajiwa kung’ara, lakini wakapotea, wachezaji waliotoka kusikojulikana na kuwa gumzo, pamoja na timu zilizoshangaza wengi kwa kile walichokionyesha.
Mwisho wa yote, Simba Queens wakawa mabingwa kwa mara nyingine, wakifanya hivyo kwa rekodi ya kuvutia ya kutopoteza hata mchezo mmoja katika mechi 22 walizocheza. Simba ilishinda mechi 19 na kutoka sare tatu, jambo linaloonyesha namna ilivyokuwa timu bora zaidi msimu huu. Lakini nyuma ya mafanikio hayo kulikuwa na hadithi nyingi zilizofanya msimu huu kuwa mmoja wa misimu yenye mvuto mkubwa katika soka la wanawake Tanzania.
WALIOTABIRIWA MAMBO YAKAWA TOFAUTI
Kabla ya msimu kuanza, jina la Cynthia Musungu Shilwatso lilikuwa miongoni mwa majina yaliyokuwa yakitajwa zaidi.
Simba Queens walimsajili akiwa na wasifu mkubwa na uzoefu wa kucheza soka la kiwango cha juu barani Afrika na Ulaya.
Mkenya huyo aliingia Tanzania akiwa tayari amejitengenezea heshima. Akiwa na Vihiga Queens aliwahi kushinda mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya kati ya mwaka 2017 hadi 2019. Baadaye akahamia Hispania katika klabu ya EDF Logrono kabla ya kurejea Afrika na kujiunga na Fountain Gate ambako aliendelea kuonyesha kiwango bora.
Baada ya kutimka Fountain akajiunga na Kryvbas ambapo alicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa wanawake na kufunga mabao saba katika mechi 16 za ligi.
Kutokana na historia hiyo, wengi waliamini angekuwa miongoni mwa wachezaji watakaotikisa ligi. Ingawa alikuwa na mchango kwenye ubingwa wa Simba, kiwango chake hakikuwa kikubwa kama matarajio ambayo wengi walikuwa wameyaweka kabla ya msimu kuanza. Kilichomrudisha nyuma ni majeraha yaliyomfanya acheze mechi chache akifunga bao moja.
Mwingine aliyebeba matarajio makubwa alikuwa mshambuliaji wa JKT Queens, Stumai Abdallah. Baada ya msimu uliopita kumaliza akiwa mfungaji bora akifunga mabao 28, mashabiki wengi walitarajia kuona msimu mwingine wa moto kutoka kwake. Wapo waliokwenda mbali zaidi na kudhani angevunja rekodi yake mwenyewe.
Hata hivyo, majeraha yakawa adui yake mkubwa. Msimu uliogeuka kuwa mgumu ulimfanya kucheza mechi tisa pekee na kufunga bao moja tu. Takwimu hizo ni tofauti kabisa na zile alizoonyesha msimu uliopita na zinaeleza kwa nini JKT Queens walikosa makali waliyokuwa nayo kwenye safu ya ushambuliaji.
Kwa upande wa JKT Queens, Najat ambaye amekuwepo kikosini hapo muda mrefu alitarajiwa kufanya makubwa kutokana na kuwa na muendelezo mzuri wa kiwango chake.
Kwa misimu mitatu mfululizo alikuwa amemaliza ligi akiwa ameruhusu mabao matatu pekee, rekodi iliyomfanya aonekane kama ukuta usiovunjika. Lakini safari hii mambo yalikuwa tofauti. Alimaliza msimu akiwa ameruhusu mabao saba, idadi ambayo inaonyesha wazi namna ushindani ulivyoongezeka.
BRICE ZANGA, USAJILI ULIOGEUKA DHAHABU
Kama kuna mchezaji aliyefanya watu wengi kubadilisha mtazamo wao msimu huu basi ni Brice Zanga wa Simba Queens.
Ulikuwa usajili ulioonekana wa kawaida kutokana na jina lake alijiunga akitokea Eclair De Sa’a ya Cameroon bila makelele makubwa ya usajili.
Wengi walizungumza zaidi kuhusu majina mengine yaliyowasili Msimbazi, lakini kadri msimu ulivyoendelea Zanga akageuka kuwa moja ya nguzo muhimu zaidi za timu.
Kiasili ni kiungo na beki wa kushoto, lakini kutokana na matatizo ya majeraha yaliyomkumba beki wa kati Ester Mayala, mara kadhaa alitumika kama beki wa kati na kufanya kazi hiyo kwa kiwango cha juu.
Ubora wake haupo tu kwenye kuzuia mashambulizi. Ana uwezo mkubwa wa kusoma mchezo, kuziba mianya kabla hatari haijatokea na kushinda mapambano ya moja kwa moja. Lakini kinachomtofautisha zaidi ni namna anavyosaidia timu kujenga mashambulizi kutoka nyuma.
ASHA MWALALA
Katika orodha ya walioshangaza wengi, jina la Asha Mwalala haliwezi kukosekana.
Msimu uliopita akiwa Simba Queens alipata wakati mgumu kupata nafasi kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo kwenye safu ya ushambuliaji.
Alirejea kutoka mapumziko ya uzazi na kukuta nyota kama Jentrix Shikangwa na Aisha Mnunka wakiwa katika kiwango bora.
Wengi walidhani safari yake ya soka la ushindani wa juu ilikuwa imefika mwisho.
Lakini alipojiunga na JKT Queens msimu huu, Mwalala alianza kuonyesha ubora wake. Alifunga mabao matano kwenye ligi na mengine matatu kwenye mashindano ya Cecafa.
Kiwango alichoonyesha kimemfanya kocha wa Timu ya Taifa, Bakari Shime kumjumuisha kwenye kikosi cha Twiga Stars kitakachoweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Wafcon. Kurejea katika kiwango hicho baada ya mapumziko ya uzazi si jambo rahisi.
ELIZABETH JOSEPH
Miongoni mwa nyota chipukizi ni Elizabeth Joseph wa Simba Queens.
Alitua Simba akitokea Alliance Girls akiwa hana presha kubwa ya matarajio. Wengi walimchukulia kama mchezaji atakayesaidia baadae, lakini ndani ya muda mfupi akawa mchezaji muhimu.
Kiungo huyo alionyesha ukomavu mkubwa katika mechi muhimu. Alikuwa na mchango mkubwa kwenye michezo dhidi ya Yanga Princess na JKT Queens, mechi ambazo mara nyingi huamua mwelekeo wa ubingwa.
Kujiamini kwake, uwezo wa kukaa na mpira na kucheza kwa utulivu vilimfanya kuwa moja ya wachezaji waliofanya sapraizi kubwa Msimbazi.
YANGA PRINCESS KUNA KITU, LAKINI…
Kwa miaka ya karibuni, Yanga Princess imekuwa ikipewa sifa kwa uwekezaji wake mkubwa kuanzia benchi la ufundi, wachezaji na namna wanavyopata huduma zinazoendana na timu ya wakubwa ikiwemo hadi kutumia usafiriwa ndege kwenye mechi za ndani.
Kikosi hicho kina baadhi ya wachezaji bora katika ligi na kimeendelea kuongeza nguvu kwa kusajili majina makubwa kutoka ndani na nje ya nchi, akiwemo Akudo Ogbonna aliyetokea Sweden.
Kwa takwimu, Yanga imeonyesha maendeleo makubwa. Msimu uliopita ilipoteza mechi zote nne dhidi ya Simba Queens na JKT Queens.
Lakini safari hii mambo yalibadilika.
Walipoteza mechi mbili pekee dhidi ya Simba Queens, wakatoa sare ya 1-1 dhidi ya JKT Queens na kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya wanajeshi hao nyumbani kwao Mej General Isamuhyo.
Tatizo kubwa linaloonekana kwa Yanga si ubora wa wachezaji. Wana vipaji vya kutosha kushindana na yeyote. Changamoto ipo kwenye usimamizi wa mechi kubwa.
Katika mbio za ubingwa, kuna michezo ambayo haihitaji kucheza vizuri bali inahitaji mipango maalumu ya kushinda. Simba na JKT wamekuwa wakifanya vizuri katika eneo hilo kwa miaka ya karibuni.
Yanga bado wanaonekana kucheza kwa ubora wa kawaida wa timu yao badala ya kubadilika kulingana na mahitaji ya kila mechi kubwa. Wakifanikiwa kuboresha eneo hilo, wanaweza kuwa tishio kubwa zaidi msimu ujao.
NIDHAMU YAILIZA JKT QUEENS
Kama kuna timu iliyojiumiza yenyewe msimu huu basi ni JKT Queens. Mbali na kushuka kwa kiwango kwa baadhi ya nyota wake, suala la nidhamu ni miongoni mwa tatizo kubwa.
Wachezaji kadhaa wa timu hiyo walipata adhabu mbalimbali kutokana na matukio tofauti yaliyotokea katika michezo ya ligi.
Donisia Minja na Alia Fikiri walifungiwa michezo mitatu kila mmoja pamoja na kutozwa faini baada ya makosa dhidi ya waamuzi. Najat Abbas na Winfrida Gerald pia walikumbana na adhabu nzito zaidi zilizowafanya kukosekana katika baadhi ya michezo mitano.
Hata mwanasaikolojia wa timu, Naomi Kaniki, alipata adhabu ya kufungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa miezi sita.
Athari za adhabu hizo zilionekana wazi ndani ya uwanja. JKT walipoteza baadhi ya wachezaji muhimu katika kipindi ambacho walikuwa wakipambana kutetea ubingwa wao.
Ni vigumu kushindana na Simba Queens ambayo ilikuwa na ubora mkubwa.
TAUSI FC WAGENI WALIOTUA NA KASI
Kati ya timu nne zilizopanda daraja msimu huu, Tausi iliyonyesha ubora kwenye msimu wake wa kwanza wa ligi. Geita Queens, Ruangwa Queens na Bilo Queens zilipanda baada ya kufanya vizuri kwenye ligi daraja la kwanza.
Tausi ilimaliza katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 29, jambo ambalo si wengi walilitarajia mwanzoni mwa msimu kwani kati ya timu hizo .
Siri kubwa ya mafanikio yao ilikuwa kwenye usajili.Tausi walivuta wachezaji wenye uzoefu mkubwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika. Fatoumata Diara na Adiaratou Coulibaly kutoka Mali, Chelsea Ngole kutoka Cameroon, Judicael Ouba na Mounifatou Helbi kutoka Burkina Faso pamoja na Matoba Cisse kutoka Ivory Coast waliongeza ubora mkubwa ndani ya kikosi hicho.
Mbali na usajili wa wachezaji wenye ubora mkubwa timu hiyo pia inafundishwa na makocha wenye uzoefu mkubwa Afrika akiongozwa na kocha mkuu, Martin Hammel raia wa Ujerumani ambaye aliwahi kufanya kazi kama kocha msaidizi kwenye timu za vijana za Ujerumani.
SIMBA QUEENS ILISTAHILI UBINGWA
Yote kwa yote Simba Queens ilistahili kunyakua ubingwa wa ligi kutokana na kuonyesha kiwango bora msimu huu.Timu hiyo ilitengeneza kikosi chenye ubora na uthubutu mkubwa. Walikuwa na safu imara ya ulinzi, viungo waliotawala mechi nyingi na washambuliaji walioweza kuamua matokeo.
Kutopoteza mechi hata moja katika mechi 22 ni jambo linalothibitisha ukubwa wa mafanikio yao. Rekodi hiyo haiji kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya maandalizi, usimamizi mzuri wa kikosi na ubora wa wachezaji.
Msimu huu umeonyesha wazi kuwa soka la wanawake Tanzania linaendelea kukua kwa kasi. Simba Queens wamechukua ubingwa, lakini Yanga Princess wanaonyesha dalili za kuimarika, JKT Queens bado wana kikosi chenye uwezo wa kurejea kwenye kiwango chao, huku Tausi FC wakithibitisha kuwa wanaweza kuwa na ubora mkubwa.
WASIKIE WENYEWE
Kocha wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka anasema “Tulikuwa na msimu sio mzuri kwa sababu tulikuwa kwenye kiwango tukashindwa kuwa na muendelezo kuna baadhi ya makosa tuliyafanya na tunaamini viongozi watayafanyia kazi.”
Kocha wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ anasema “Kulikuwa na presha kubwa kwa sababu kila timu ilikuwa inakuja kwa ajili ya kupata matokeo kwa sababu hatukupoteza mechi lakini tunashukuru tulikuwa na muendelezo mzuri hadi mwisho wa msimu tukawa mabingwa.”