MVUTANO URENO? DADA WA RONALDO AIBUA TAHARUKI MPYA
LISBON, Ureno: DAMU nzito… Dada yake Cristiano Ronaldo ameonekana kuunga mkono chapisho la Instagram lililomkosoa Bruno Fernandes, jambo ambalo limezua ya uwezekano wa mvutano ndani ya kambi ya Ureno baada ya sare ya 1-1 dhidi ya DR Congo Jumatano.
Ureno iliwasili nchini Marekani ikiwa miongoni mwa timu zilizotajwa kuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika Kombe la Dunia, lakini ilianza kampeni yake kwa matokeo ya kukatisha tamaa mjini Houston.
Joao Neves aliipa Ureno bao la mapema kwa bao la kichwa, lakini kabla ya mapumziko Yoane Wissa aliisawazishia DR Congo.
Matokeo hayo yalibaki hadi mwisho wa mchezo licha ya Ureno kuwa juu kwa nafasi 37 katika viwango vya dunia vya FIFA.
Dada ya Ronaldo amezua mjadala
Baada ya matokeo hayo, ukosoaji mkubwa umeibuka nchini Ureno, huku baadhi ya mashabiki wakitaka Ronaldo aondolewe kikosini baada ya kushindwa kupiga hata shuti moja lililolenga lango katika mchezo huo.
Lakini hali ilichukua sura mpya baada ya dada mkubwa wa Ronaldo, Katia Aveiro, kuonekana akipenda (like) chapisho la Instagram kutoka ukurasa mmoja wa Brazil uliomkosoa Bruno Fernandes.
Chapisho hilo lilidai kuwa Fernandes huonyesha kiwango bora akiwa na Manchester United lakini hashindwi kuonyesha kiwango hicho akiwa na timu ya taifa ya Ureno.
Pia lilimlinganisha na Raphinha wa FC Barcelona, ambaye amekuwa akikosolewa kutokana na kiwango chake akiwa na timu ya taifa ya Brazil.
Ronaldo ndiye anayekosolewa zaidi
Licha ya hilo, Ronaldo mwenyewe ndiye aliyepokea lawama nyingi zaidi baada ya kuonekana kuwa mbali na kiwango chake cha zamani.
Mshambuliaji huyo wa Al Nassr FC aligusa mpira mara 25 pekee dhidi ya DR Congo na hakutengeneza nafasi yoyote ya wazi ya kufunga, lakini bado hakutolewa nje ya uwanja.
Dakika ya 83, wakati Ureno ikihitaji bao la ushindi, kocha Roberto Martinez alimtoa Vitinha na kumuingiza Goncalo Ramos badala ya kumtoa Ronaldo.
Hatua hiyo ilikosolewa vikali na mshambuliaji wa zamani wa England, Chris Sutton.
“Martinez anaogopa kumtoa. Yeye si meneja halisi wa timu. Ronaldo anaweza kufunga bao la ushindi, lakini mchezo ulimpita kabisa,” alisema Sutton.
Aliendelea kusema: “Ronaldo alikuwa mchezaji wa kutengeneza nafasi zamani, lakini sasa ni mfungaji wa mwisho tu. Sioni mantiki katika baadhi ya uamuzi ya Martinez. Ronaldo alikuwa pembeni kabisa mwa mchezo na Martinez anatakiwa kuwa jasiri vya kutosha kuonyesha kwamba yeye ndiye kocha.”
Martinez amtetea Ronaldo
Martinez alijibu ukosoaji huo kwa kusisitiza kuwa haikuwa na mantiki kumtoa mfungaji bora wa muda wote wa Ureno wakati timu yake ilikuwa ikihitaji bao.
“Tulikuwa tunapata shida kwa sababu walikuwa wanacheza kwa mabeki wengi nyuma,” alisema.
“Katika hali kama hiyo unaweza kutumia sifa za Cristiano. Haina mantiki kumtoa mchezaji kama Cristiano Ronaldo wakati unahitaji mabao.
“Namna anavyovuta mabeki na kutumia nafasi ni jambo lenye thamani kubwa. Unapohitaji mabao, unahitaji mchezaji kama Cristiano Ronaldo awe uwanjani.”
Martinez kuelekea Al Nassr?
Mashindano haya ya Kombe la Dunia yanatarajiwa kuwa ya mwisho kwa Martinez kuinoa Ureno, huku ripoti zikidai kwamba ana mazungumzo na Al Nassr FC kuhusu uwezekano wa kuhamia Saudi Arabia.
Klabu hiyo inatafuta kocha mpya baada ya kuondoka kwa Jorge Jesus mwezi uliopita baada ya kushinda ubingwa wa ligi.
Awali ilidhaniwa kuwa Al Nassr ilimlenga Marco Silva, lakini taarifa zinaonyesha huenda akaelekea SL Benfica.
Iwapo Martinez atajiunga na Al Nassr, ataungana tena na Ronaldo mjini Riyadh pamoja na Joao Felix, ambaye pia yupo na kikosi cha Ureno katika Kombe la Dunia nchini Marekani.