YANGA na Simba zimepigwa bao na Azam FC kuinasa saini ya nyota wa Kagera Sugar, Kassim Khamis ambaye amesaini kandarasi ya miaka miwili ndani ya mabosi wa Dar es Salaam ambao kwa sasa wapo nchini Rwanda.
Yanga na Simba walikuwa vitani kuwania saini ya nyota huyo mwenye uwezo wa kucheka na nyavu kila anapopata nafasi pamoja na uwezo wake wa kukaa na mpira akiwa uwanjani.
Akizungumza na Saleh Jembe, Kassim amesema kuwa kilichomfanya asaini Azam FC ni maslahi bora pamoja na uwekezaji wa Azam FC.
“Mimi ni mchezaji sichagui kambi, nilikuwa nazungumza na timu nyingi kabla sijatua hapa ikiwa ni pamoja na Simba, Yanga hata mabosi wangu Kagera Sugar nao nimezungumza nao ila mwisho wa siku nimetua hapa.
“Kikubwa cha kufanya ni kufikiria changamoto mpya na kupambana ili kufikia malengo yangu mambo mengine yatafuata,” amesema Kassim.