MWAMUZI aliyechezesha mechi ya watani wa jadi, Jonesia Rukya na beki wa Simba, Pascal Wawa wanatarajiwa kujadiliwa katika Kamati ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na matukio yaliyojitokeza katika mechi ya watani wa jadi baina ya Simba dhidi ya Yanga.
Kumekuwa na malalamiko juu ya mwamuzi huyo kutoa penalti isiyo halali katika mechi ya watani wa jadi kwa upande wa Simba iliyofungwa na Meddie Kagere ambaye inaonekana ni kama alivutwa nje ya boksi na beki wa Yanga, Kelvin Yondani lakini aliangukia ndani na mwamuzi kuamuru iwe penalti, jambo ambalo limezua utata hadi sasa.
Aidha, kwa upande wa Wawa katika mchezo huo alionekana akimkanyaga kwa makusudi mshambuliaji wa Yanga, Ditram Nchimbi katika harakati za kuokoa mpira.
Championi Ijumaa lilizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto ambapo alisema kuwa, kuna matukio mbalimbali ambayo yamejitokeza katika mechi za hivi karibuni, hivyo Kamati ya Saa 72 ya TFF inatarajiwa kukaa hivi karibuni kwa ajili ya kupitia matukio hayo na kuyatolea ufafanuzi na kutoa adhabu pale panapostahili.
“Kikao cha Saa 72 bado hakijakaliwa hadi sasa, kuna matukio mengi yamejitokeza katika mechi za hivi karibuni, hivyo masuala yote hayo yatafi kishwa katika kamati hiyo na kuangaliwa na kutolewa ufafanuzi.
“Hivyo, kwa sasa hakuna majibu ya moja kwa moja hadi kamati hiyo itakapopitia mechi zote na kijiridhisha na kile kilichotokea yakiwemo matukio ya mechi ya Simba na Yanga,” alisema Mguto.