UONGOZI wa Azam FC umesema utamuongezea mzigo wa machungu, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael ambaye alipokea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Kagera Sugar ikiwa ni mchezo wake wa kwanza akiwa kwenye benchi la ufundi akipokea mikoba ya Mwinyi Zahera.
Mchezo wake wa kwanza ulichezwa Januari 15, Uwanja wa Uhuru, kesho,Januari 18 atakuwa tena Uwanja wa Taifa kumenyana na Azam FC.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Maganga amesema kuwa wanatambua kazi inayofuata itakuwa dhidi ya Yanga hawana hofu na hilo kwani wana nguvu na morali ya kutosha.
“Ushindi wetu wa mabao 2-0 mbele ya Lipuli tunaachana nao sasa jambo jingine jipya ni kushinda mbele ya Yanga, tunawaheshimu wapinzani wetu ila tunazihitaji pointi tatu zao zina umuhimu kwetu, kama ambavyo wao wanazitaka” amesema Maganga.
Azam FC iliyo chini ya Arstica Cioaba imejikusanyia jumla ya pointi 29 ikiwa nafasi ya tatu imecheza jumla ya mechi 14, itacheza na Yanga iliyocheza mechi 13 na pointi 25 kibindoni.