Mlinzi wa klabu ya Yanga, Ally Mtoni ameomba msamaha kufuatia kitendo cha kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Azam FC katika mchezo wa ligi.
Mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, ulishuhudia Yanga ikipoteza kwa bao 1-0, ambapo Ally Mtoni alimkanyaga mchezaji wa Azam FC katika kipindi cha pili na kupelekea kupewa kadi nyekundu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mtoni ameandika, “naomba msamaha kwa wanamichezo wote kwa kadi niliyoipata siku ya jana (juzi) na tukio nililofanya kwenye mchezo wetu dhidi ya Azam FC, kweli mchezo wa mpira ni mchezo wa furaha na upendo kwa kuwa ni ajira ila changamoto za hapa na pale zipo”, amesema Ally Mtoni.
“Pia naomba msamaha kwa wachezaji, viongozi wangu wa Yanga SC na pia hata wa Azam FC na hata viongozi wenye dhamana na soka letu TFF, sitaweza kuja rudia tukio la aina ile”, ameongeza.
Yanga sasa imecheza jumla ya michezo 14 katika ligi, ikiwa na pointi 25. Imepoteza mchezo wa pili mfululizo chini ya kocha mpya, Luc Eymael, ambapo mchezo wa kwanza ilifungwa na Kagera Sugar Jumatano, Januari 16.