Mtandao unaojihusisha na masuala ya data na fursa za kimtandao kwa wanamichezo, vilabu na mashirikisho wa ‘Result Sports’ wenye makao makuu mjini Büdingen nchini Ujerumani umetoa listi ya klabu za soka zenye wafuasi wengi duniani katika mtandao ya kijamii.
Data hizo zilizotolewa mwezi Januari 2020 zinaonesha kuwa Barcelona inaongoza duniani kuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni 260 kutoka katika mitandao yake ya Instagram, Twitter, Facebook, YouTube na milioni 8 kutoka mitandao mingine.
Real Madrid inakamata namba mbili ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni 258, Manchester United ikishika namba tatu ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni 142. Chelsea ina wafuasi zaidi ya milioni 93 katika nafasi ya nne huku Juventus ikishika namba tano kwa wafuasi zaidi ya miloni 90, nafasi ya sita ni Bayern Munich, Liverpool nafasi ya saba, PSG nafasi ya nane, Man City nafasi ya tisa na Arsenal nafasi ya 10.
Kwa klabu za Afrika, mabingwa mara nane wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Al-Ahly inaongoza kwa wafuasi wengi ikiwa na zaidi ya wafuatiliaji milioni 25, ikishika namba 18 duniani. Nafasi ya pili kwa Afrika inafuatiwa na Zamalek iliyo na wafuasi zaidi ya milioni 11 huku ikishika nafasi ya 32 duniani.
Kwa Afrika Mashariki inaongozwa na klabu ya Simba ambayo imeingia kwa mara ya kwanza katika listi hiyo, ambayo imeshika nafasi ya 151 duniani huku ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni moja. Facabook ina wafuasi zaidi ya 568,000, Instagram ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni 1, Twitter ina wafuasi takribani 142,000 na YouTube ikiwa na wafuasi zaidi ya 21,000.
CREDIT: EAST AFRICA TV