KIKOSI cha Simba Jana kimebanwa mbavu Uwanja wa Uhuru mbele ya JKT Tanzania kwa kufungwa bao 1-0 mchezo wa Kwanza wa mzunguko wa pili msimu wa 2019/20.
Simba iliyo chini ya Kocha Mkuu, Sven Vanderbroeck ilifungwa bao dakika ya 24 kupitia kwa mshambuliaji wa JKT Tanzania, Adam Adam aliyefunga bao hilo kwa kichwa kilichozama nyavuni na kumshinda mlinda mlango, Beno Kakolanya.
Licha ya Simba kuongeza juhudi za kusaka ushindi kipindi cha pili mabao yalikuwa magumu kwani walishindwa kufurukuta mbele ya JKT Tanzania ambao walikuwa na spidi kubwa mwanzo mwisho.
Kipindi cha pili Simba ilifunga bao kupitia kwa Gerson Fraga dakika ya 52 mwamuzi alisema kuwa ni bao la kuotea kwa Simba.
Licha ya Simba kufanya mabadiliko kwa kumtoa Ibrahim Ajibu nafasi yake ikachukuliwa na John Bocco, Francis Kahata kuchukua nafasi ya Shiza Kichuya na Gerson Fraga nafasi yake kuchukuliwa na Clatous Chama bado mambo yalikuwa magumu.
Nyota mpya wa Simba Luis alionyesha makeke kwa mara ya kwanza kwa dakika tisini huku Kichuya akicheza kwa dakika 45 ndani ya Uwanja.
Simba inabaki nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 50 na leo itakuwa zamu ya Yanga Uwanja wa Uhuru dhidi ya Ruvu Shooting.
Huu unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Sven kuambulia kichapo akiwa kwenye bechi baada ya kupokea mikoba ya Patric Aussems aliyepigwa chini jumla.
Sven amesema kuwa sababu kubwa ya kushindwa kupata matokeo ni washambuliaji kutokuwa makini kutumia nafasi walizopata pamoja na kuwa na wachezaji wengi majeruhi.