MWADUI FC, Mbeya City, Mbao FC na Singida United zinateswa na upepo mbaya wa kupambania nafasi zao za kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri msimu huu wa 2019/20.
Timu nne za mwisho kuanzia itakayoshika nafasi ya 17-20 zitashuka daraja jumlajumla msimu huu huku zile mbili zitakazokuwa nafasi ya 15 na 16 zitacheza playoff na atakayefungwa anashuka kwa kuwa msimu wa 2020/21 zitashiriki timu 18 pekee.
Mbao FC iliyo chini ya Kocha Mkuu Hemed Morocco ipo nafasi ya 17 imeshinda mechi nne,sare saba na kupoteza tisa Kati ya mechi 20 ilizocheza na pointi zake 19.
Mwadui FC ipo nafasi ya 18, msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja na ikiishia kucheza playoff na Geita Gold ilishinda mabao 2-0 kwa sasa ina pointi 18 sawa na Mbeya City ya Amri Said ikiwa imecheza mechi 21 nafasi ya 19.
Singida United ya Ramadhan Nswanzurimo inafunga majalada ya wote ikiwa nafasi ya 20 imecheza mechi 21 imeshinda mbili, kupoteza 14 na sare tano.
Kocha wa Mbeya City,Said amesema kuwa watapambana kupata matokeo kwenye mechi zilizobaki ili kubaki ndani ya ligi kwani nafasi bado ipo.