KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael amesema kuwa ana imani kikosi chake kitamaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara katika nafasi ya pili inayoshikiliwa na Azam FC yenye pointi 54.
Eymael amesema kuwa itakuwa ni kujiongopea kwa sasa akisema kuwa anahitaji kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na kuachwa na wapinzani wake Simba ambao wapo nafasi ya kwanza.
Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 71 baada ya kucheza mechi 28 huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu na ina pointi 51 baada ya kucheza mechi 27.
Namungo FC ipo nafasi ya nne ikiwa imejiwekea kibindoni pointi 50.
Eymael amesema: “Ninatambua kwamba mashabiki wanahitaji kuona timu inatwaa ubingwa lakini kwa sasa malengo yangu makubwa ni kuona timu inamaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
“Hilo lipo mkononi mwetu ukizingatia kwamba wachezaji wamekuwa na morali nzuri na maendelea yanaonekana nina amini kwamba kila mmoja atafurahi kuona namna ambavyo tutafikia malengo tuliyojiwekea,” amesema.
Yanga imebakiza mechi 11 mkononi ili kumaliza ligi ambayo imesimama kwa muda kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona.