WINGA wa Simba, Shiza Kichuya alisajiliwa na timu hiyo wakati wa usajili wa dirisha dogo na mpaka sasa amecheza michezo miwili dhidi ya JKT Tanzania na Stand United.
Mechi ya JKT Tanzania ilikuwa ni ya Ligi Kuu Bara na Stand United ulikuwa mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA).
Katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania Kichuya alicheza dakika 45, za kipindi cha kwanza na kutolewa ambapo mechi ya FA alicheza dakika 62 hivyo kumfanya acheze dakika 107 mpaka sasa.
Kichuya amesema hana wasiwasi wowote kwani anatambua kuwa ameshindwa kucheza mechi nyingi kutokana na utimamu wake wa mwili haukuwa sawa na alikuwa nje ya uwanja zaidi ya miezi minne iliyomfanya uzito wake uongezeke.
Amesema sasa hivi yupo nyumbani kwao Morogoro mbali ya kufanya mazoezi ambayo wamepewa na kocha wao lakini hutumia muda wake kufanya mzoezi binafsi yanayomrudisha katika hali yake ya ushindani.
“Nafahamu kuna maneno mengi huko mtaani lakini kwangu wala sijali nafahamu jambo ambalo limenikwamisha wakati najiunga na Simba mpaka kushindwa kucheza mechi nyingi, ligi ikirejea watamuona Kichuya aliyekuwa ametoka Mtibwa Sugar kujiunga na Simba,”
“Mimi mwenyewe huwa najifahamu nikiwa fiti wala sitaki mtu, kocha au mchezaji mwenzangu aniambie nipo tayari kwa kushindana ila ambavyo najiona wakati huu kweli naenda kufanya kazi ndani ya timu na kutoa mchango wangu,” amesema Kichuya.