Home Uncategorized SENZO AFUNGUKA ATAKAVYOWARUDISHA BONGO KAGERE, CHAMA NA SHIBOUB

SENZO AFUNGUKA ATAKAVYOWARUDISHA BONGO KAGERE, CHAMA NA SHIBOUB

WAKATI mipaka ya nchi zao ikifungwa, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Senzo Mazingisa amepanga kuandaa utaratibu wa tofauti watakaoutumia ili kuhakikisha nyota wao wa kimataifa waliopo nje ya Tanzania wanarejea kwa wakati nchini.

 Wachezaji wa Simba waliopo nje ya Tanzania ni Francis Kahata, Meddie Kagere, Sharraf Eldin Shiboub, Luis Miquissone na Clatous Chama ambao kati ya hao mipaka ya nchi zao imefungwa ili kuzuia na kupunguza maambukizi ya Virusi vya Corona.

 Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hivi karibuni lilitangaza kusogeza mbele tarehe ya kuendelea kwa mechi za msimu huu, hiyo ni baada ya maambukizi hayo kuongezeka ambayo hivi sasa itaanza Juni 30 na siyo Mei 30, mwaka huu kama ilivyopangwa awali.

Akizungumza na gazeti la Championi Ijumaa, Senzo alisema kuwa utaratibu huo utakaotumika kuwarejesha nyota wao wa kimataifa wamepanga kuuanza mapema na hivi karibuni watautangaza, lengo ni kuona wachezaji wote wanarejea kwa wakati ili kuendana na program ya kocha atakayoianza.

 Senzo alisema wachezaji wao walisafiri kabla ya tamko la Serikali ya Tanzania baada ya kupokea barua kutoka timu zao za taifa, hivyo wanalazimika kufanya kila liwezekanalo ili wachezaji wao warudi kwa wakati.

 Aliongeza kuwa lengo lao ni kutimiza amri ya serikali waliyoitoa ya kukaa karantini kwa siku 14 kabla ya kuungana na wenzao katika mazoezi ya pamoja huku wakiisubiria ligi kuanza hiyo Juni, mwaka huu.

 “Kuhusiana na wachezaji wetu waliosafiri nje ya Tanzania, kabla ya mechi zetu mbili za Azam FC na Yanga, tulipokea barua za wachezaji kuhitajika na timu zao za taifa kwa ajili ya kufuzu michuano ya Afcon.

 “Hivyo, kama uongozi tulipokea barua hizo kutoka Kenya, Zambia, Rwanda, Msumbiji, Sudan na kama tungewazuia tungeadhibiwa na Fifa, hivyo tukaona ni vema tuwaruhusu na ndiyo kitu tulichokifanya kuwaruhusu kwenda kuzitumikia timu zao za taifa.

 “Kabla ya kuwaruhusu wachezaji wetu hao, Serikali ya Tanzania ilikuwa bado haijatoa maamuzi juu ya janga la Corona kuwa wageni wakifika lazima waingie karantini kwa hiyo kwa sasa tunaangalia njia gani tutakazozitumia kuwarudisha kwa wakati ili wakakae karantini halafu wajiunge na timu,” alisema Senzo.

SOMA NA HII  AZAM FC YAWAITA MASHABIKI AZAM COMPLEX KUONA BURUDANI