KATIKA kuhakikisha inatekeleza mapendekezo ya kukiimarisha kikosi chao kama ilivyopendekezwa na Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, uongozi wa Yanga umeanza mchakato wa kunasa saini ya mshambuliaji, Jimmy Ukonde kutoka UD Songo ya Msumbiji.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz alisema uamuzi wa kumsajili Ukonde unatokana na ripoti ya benchi la ufundi la timu hiyo ambayo inahitaji kuimarisha safu hiyo ya ushambuliaji.
Nugaz alisema mazungumzo kati Yanga na Ukonde yanaendelea vema na wanaamini asilimia 90 nyota huyo ambaye amewahi kucheza na winga wa Simba, Luis Miquissone atatua nchini kujiunga na klabu yao.
Alisema klabu imejipanga kukamilisha vema mchakato huo wa usajili kwa kushirikiana na wadhamini wao, Kampuni ya GSM ili malengo ya kutwaa ubingwa katika msimu ujao yatimie bila shaka.
“Baada ya viongozi na mdhamini GSM kukutana na kujadili mambo mbalimbali, ikiwamo suala la usajili, sasa macho yetu tunayaelekeza katika kumsajili, Jimmy Ukonde, ni kifaa ambacho kitakuja kuibeba Yanga, tunawaambia wajiandae, ” alisema Nugaz.
Aliongeza kuwa Eymael amerishindwa na kiwango cha Ukonde baada ya kumfuatilia kwenye mechi za hivi karibuni alizocheza akiwa na klabu yake.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema pia klabu inaendelea na mazungumzo ya kuwaongezea mikataba wachezaji wao ambao mikataba yao ya awali inaelekea ukingoni na Eymael bado anahitaji huduma zao.
“Wakati tunaendelea na mipango ya kusaka wachezaji wapya, pia tunafanya mazungumzo na wachezaji wa zamani ambao kocha amependekeza tuwabakishe, nafasi kubwa tunayoipa kipaumbele ni ya ushambuliaji,” Mwakalebela alisema.
Yanga pia inatajwa kuwinda saini ya nyota wawili kutoka Polisi Tanzania ambao ni kiungo, Baraka Majogoro na beki wa kati, Yassin Mustapha.
Hata hivyo wachezaji hao bado wana mikataba na timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Polisi.