WAKALA wa kimataifa wa soka nchini, Ally Saleh amefichua kuwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ana nafasi kubwa ya kubaki katika Ligi Kuu ya England hata ikitokea timu yake Aston Villa itashuka daraja.
“Kuna kampuni ya uwakala ambayo nimekuwa nawasiliana nayo kwa ukaribu imenihakikishia kuwa upo uwezekano wa Samatta kununuliwa hadi kwa dau la Sh 50 bilioni (Pauni 17.3 milioni) kutegemeana na jinsi wao watakavyoweza kufanya ushawishi wao.
“Unajua nguvu ya uwakala ina nafasi kubwa katika kusaidia mauzo ya mchezaji lakini pia kupandisha thamani yake. Ninaweza kusema biashara ya wachezaji ni kama ya kimafia, sasa kama hauna wakala mwenye ushawishi mkubwa kwa timu mbalimbali, unaweza kuwa na mchezaji mzuri na asinunulike na unaweza kuwa na mchezaji wa kawaida akawa na soko tena kwa gharama kubwa.
“Tayari nimeshazungumza na wawakilishi wa Samatta kuona ni kwa namna gani wanaweza kutumia fursa hiyo. Kampuni hiyo ambayo iko tayari kufanikisha hilo dili, inamiliki idadi kubwa ya wachezaji mastaa duniani hasa wa Brazili na mmojawapo ni Richarlison anayechezea klabu ya Everton,” alisema Saleh.
“Ilivyo ni kwamba kadri mchezaji anapouzwa kwa fedha nyingi ndipo wakala/mawakala wananufaika na pia ukubwa na hadhi ya ligi vina nafasi kubwa ya kuongeza thamani ya mchezaji sokoni.
“Kingine kinachopandisha thamani yake ukiondoa kiwango na umri ni yale mambo yaliyomo katika mkataba wa mchezaji. Kwa hiyo sio jambo la kushangaza ikiwa Samatta atanunuliwa kwa dau kubwa kwani klabu inakuwa ina kiwango chake ilichokiweka kwa ajili ya mauzo ya mchezaji na mawakala wao wana mbinu zao za kuipandisha.
“Kwa mfano, wakati Samatta anauzwa na Simba kwenda TP Mazembe kwa dau la Dola 150,000 mimi nilishapeleka ofa ya Dola 250,000 (Sawa na Milioni 500) kwa Simba iliyotoka katika klabu moja nchini Austria ambayo ilionyesha nia ya kumsajili Samatta. Lakini tayari walikuwa wameshafikia makubaliano na klabu hiyo ya DR Congo,” alisema Saleh.
Samatta mwenye umri wa miaka 27, alijiunga na Aston Villa wakati wa usajili wa dirisha dogo, mwezi Januari mwaka huu kwa ada ya uhamisho inayokadiriwa kufikia kiasi cha Pauni 8.5 milioni (zaidi ya Sh 16 bilioni) akitoka KRC Genk ya Ubelgiji ambayo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo msimu wa 2018/2019.
Katika mechi sita alizoichezea Aston Villa tangu alipojiunga nayo, Samatta ameifungia mabao mawili, mojawapo likiwa ni katika mechi ya fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Manchester City.