Na Mwandishi Wetu
BAADA ya Serikali ya Ujerumani kusema timu zote za Bundesliga kukaa karantini kabla ya kuanza kwa ligi tena, sasa ni uhakika kuwa Mei 16, mambo yanarejea.
Wapenda soka watarejea tena kukaa kwenye viti kushuhudia soka la kiwango cha juu likichezwa tena kupitia king’amuzi cha StarTimes ikiwa ni Bundesliga imerejea rasmi.
StarTimes wao wanajinasibu na muonekano ng’aavu wa HD lakini kwa mashabiki wa soka ni sawa na kusema “uhai umerejea”, macho yataona yanachotaka, masikio yatasikia yanachopenda, moyo utafungua milango ya furaha.
Bundesliga inakwenda kuwa ligi ya kwanza inayorejesha tena uhai wa michezo na soka dhidi ya maambukizi yanayoogofya ya Covid-19 ambayo yameisimamisha dunia.
Mechi sita za mwanzo za Bundesliga zinasimamisha tena uhai wa michezo duniani kote na kila timu hadi sasa imebaki mechi 10 kumaliza msimu.
Kila timu inakwenda kupigania uhai wake katika mechi hizo kumi na makundi ni manne kama kawaida. Moja ni lile linalotaka ubingwa, bila wale wanaotaka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, tatu wanaowania kushiriki michuano ya Europa League na nne, wanaopigania kuepuka kuteremka daraja.
Hadi sasa Bayern Munich, Dortmund, RB Leipzig, Monchegladbach na Leverkusen kila moja ina nafasi ya kuwa bingwa kulingana na itakavyozicheza hizo karata 10 zilizobaki na inaonyesha Schalke 04, Freiburg, Wolfsburg na Hoffenheim zina nafasi ya kuwania kucheza Europa League huku waliobaki ni wale wanaopambana kuendelea kubaki Bundesliga.
Mechi 10 si ndogo, zinaweza kubadilisha kila kitu, zinaweza kufanya mambo yakawa magumu au tofauti na yanavyotegemewa.
Kila mmoja lazima akomae kweli kwa kuwa rekodi za Bundesliga kwa msimu wa 2019/20 zinaonyesha ligi hiyo haina mwenyewe sana kama ambavyo awali ilinekana ni Bayern tu, akiteleza ni Dortmund.
Hata kama wanaongoza, Bayern akiwa na pointi 55, Dortmund 51 lakini unaona RB Leipzig ana pointi 50, Monchengladbach ana 49 na Leverkusen ana 47. Bado ngoma si nyepesi namna hiyo.
Jumamosi Mei 16:
Augsburg Vs Wolfsburg
Dortmund Vs Schalke 04
Dusseldorf Vs Paderborn
Hoffenheim Vs Berlin
RB Leipzig Vs Freiburg
Frankfurt Vs Monchengladbach
Jumapili Mei 17:
FC Koln Vs Mainz
Union Berlin Vs Bayern
Jumatatu Mei 18:
Bremen Vs Leverkusen