KADRI siku zinavyozidi kuyoyoma, ndivyo kikosi cha Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, kinavyozidi kuwa kitamu kiasi cha kuonekana kama hakikuwa likizo.
Shughuli za michezo nchini zilisimamishwa tangu Machi 17, mwaka huu kutokana na hofu ya kuenea kwa maambukizi ya virus vya corona.
Kwa muda wote huo wa takribani miezi mitatu, wachezaji walikuwa wamejichimbia makwao, japo wapo waliokuwa wakiendelea na mazoezi binafsi kulingana na maelekezo ya makocha wao.
Hata hivyo, kuna wachezaji ambao wanaonekana hawakuwa wakipiga tizi kutokana na kuongezeka uzito kama ilivyojionyesha mara baada ya timu kuanza mazoezi wiki iliyopita.
Japo katika kikosi cha Simba kuna wachezaji wachache mno wanaonekana kuongezeka uzito, lakini kwa yanayoendelea mazoezini kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, huwezi kuamini kama walipumzika kwa muda mrefu.
Kama ilivyojionyesha mapema wiki hii katika michezo yao miwili ya kirafiki waliyocheza kwa siku moja, wachezaji wa Simba wamekuwa wepesi huku wakipiga kazi barabara.
Katika mazoezi ya juzi na jana, wote walikuwa wakijituma hasa, wakifuata kwa umakini maelekezo ya makocha wao, Sven Vandenbroeck na msaidizi wake, Seleman Matola.
Jana asubuhi walipewa program ya kupiga pasi fupi fupi na za kasi, kama sehemu ya kuwaimarishia stamina na hata umiliki wa mpira ambapo walifanya vizuri mno kiasi cha kuwafurahisha makocha wao hao.
Zoezi hilo la pasi fupi fupi lilitumia saa moja, likilenga kujiandaa kuwavuruga wapinzani wao watakapocheza nao katika mechi zao zijazo za Ligi Kuu Bara, wakitarajiwa kuanza na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumapili hii.
Mara baada ya kumaliza programu hiyo, likaja zoezi la kupiga pasi ndefu kabla ya kumalizia lile la kufunga mabao ya mbali na karibu ya goli.
Kwa upande wa makipa, Aishi Manula, Beno Kakolanya na Ally Salim, walikiona cha moto kutokana na mashuti yaliyokuwa yakielekezwa langoni na washambuliaji wakati wa zoezi la kufunga mabao.
Baada ya mazoezi hayo, Sven aligawa vikosi viwili na kucheza mechi mazoezi ambayo kila mchezaji alionyesha kiwango ili kulishawishi benchi la ufundi kumpa namba Jumapili.
Akizungumza mara baada ya mazoezi hayo, Sven alisema kuwa tangu wachezaji wake waanze mazoezi wiki iliyopita, wamekuwa wakiendelea vizuri na hiyo imetokana na kutekeleza programu alizowapa kipindi cha likizo ya corona.
“Hadi hivi sasa timu ipo tayari kwaajili ya mechi kwa sababu kila mmoja anatimiza majukumu yake kwa ukamilifu. Katika mechi za kirafiki, nilikuwa nahitaji kupata kikosi nitakachoanza nacho mechi na Ruvu na tayari nimekipata, hivyo mashabiki waje uwanjani kuona kitu kizuri kitakachofanywa na wachezaji,” alisema.
Simba inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na alama 71 baada ya kucheza mechi 28, ikiwa imesaliwa na 10 kuhitimisha msimu huu.
Ili kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, Wekundu wa Msimbazi hao wanahitaji pointi 15 tu kutoka katika mechi zao hizo zilizobaki.
Hilo linatokana na ukweli kuwa Simba imezicha kwa mbali Azam na Yanga zinazofuatia katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20.
Wakati Azam ikiwa nafasi ya pili na pointi zao 54 baada ya kucheza mechi 28, Yanga wanafuatia kwa pointi zao 51 walizozivuna kutokana na michezo 27.