Home Uncategorized KUELEKEA ‘GAME’ YA JUMAMOSI NA MWADUI…SVEN AMEFUNGUKA HAYA…

KUELEKEA ‘GAME’ YA JUMAMOSI NA MWADUI…SVEN AMEFUNGUKA HAYA…

KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck amewaambia mashabiki kwamba mziki unaoshuka Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Mwadui ni tofauti kabisa na wataona wenyewe mabadiliko.

Lakini akakiri pia kwamba winga wake, Shiza Kichuya aliyetupia dhidi ya Ruvu Shooting juzi amekuwa mtamu kwa sasa.

Mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, Kichuya alianza katika kikosi cha kwanza na kutupia katika dakika ya 11.

Baada ya mazoezi ya jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alieleza kuwa wakati Kichuya anasajiliwa na Simba hakuwa fiti ndio maana hakuwa anamtumia.

“Nilimpa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza Kichuya ambaye alinishawishi katika mazoezi na alikwenda kufanya kama ambavyo aliagizwa pale uwanjani,” alisema.

“Kichuya alifanya vile ambavyo nilikuwa nataka kutoka kwake na akafunga bao muhimu kwetu ingawa tulishindwa kupata mengine zaidi kama ambavyo tulitegemea.

“Kimsingi Kichuya amerudi na kama ataendelea kufanya hivyo nitakuwa nampa nafasi ya kucheza tofauti na hapo awali, ameongeza ushindani katika nafasi ambayo anacheza,” alisema Sven.

WACHEZAJI WAMUANGUSHA

Katika hatua nyingine Sven, alieleza kuwa wachezaji wake wamemuangusha katika mechi ya juzi dhidi ya Ruvu Shooting ambayo walikuwa na malengo ya kuondoka na pointi tatu.

“Baadhi ya wachezaji wangu waliniangusha kwa kucheza tofauti na vile ambavyo nilikuwa tunafanya mazoezini, tulifanya mazoezi ya mbinu na nguvu nyingi kwa kutambua tunakwenda kucheza dhidi ya timu yenye matumizi zaidi ya nguvu, lakini tulipofika uwanjani wachezaji wangu walionekana kuzidiwa mara kwa mara.

“Si mbaya tumedondosha pointi mbili nyumbani na kupata moja na matatizo ambayo tumeyaona katika mchezo juu tutakwenda kuyafanyia kazi ingawa nafahamu kwa kukaa bila kuwa pamoja kwa zaidi ya miezi miwili lazima shida kama hizi zitokee,” alisema Sven.

“Tutabadilika na kuwa imara zaidi katika mechi ya Jumamosi,” aliongezea Sven.

ISHU YA JONAS MKUDE

Kiungo wa Simba, Jonas Mkude amerejea katika mazoezi ya timu hiyo ambayo yalifanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru huku wakicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Transit Camp ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mkude uwanjani hapo alikuwa chini ya kocha wa viungo, Adel Zrane aliyemuwekea kibaiskeli ambacho kilikuwa pembeni na alitakiwa kunyonga taratibu na haraka kwa dakika 15.

Baada ya hapo alifanya mazoezi mepesi ya viungo na baadaye zoezi lingine la kutembea taratibu akizunguka uwanja mzima wa Uhuru katika eneo la kukimbilia.

Baada ya kumaliza mazoezi hayo, Mwanaspoti ilimfuata Mkude na kueleza kuwa anaendelea vizuri na matibabu ambayo aliyaanza muda mfupi mara baada ya kuumia.

“Matibabu ambayo napata yamenifanya kuendelea vizuri mpaka kuwa na matumaini mkubwa yaani kabla ya wiki mbili kumalizika nitakuwa nipo fiti kwa mashindano,” alisema.

“Zile wiki mbili ambazo zilielezwa ni kufanya matibabu pamoja na mazoezi mepesi ya kunirudisha katika bali yangu ya ufiti ambayo nina imani siku si nyingi nitakuwa sawa kwa ambavyo najioni.

“Vipimo ambavyo nilifanya havikuonyesha tatizo kubwa bali ni mishtuko midogo midogo ambayo muda si mwingi nitakuwa fiti,” alisema Mkude.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema hali ya Mkude si rahisi kueleza moja kwa moja mpaka hapo atakapopata ripoti maalumu kutoka kwa jopo na madaktari ambalo linamfuatilia.

Mkude aliumia katika mechi ya kirafiki dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena wiki iliyopita ambayo Simba ilishinda 3-1.

WAWAPIGA WAJEDA

Katika hatua nyingine juzi Simba ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Transit Camp na kuipiga mabao 4-0 yaliyofungwa na Ibrahim Ajibu, Gerson Fraga aliyefunga mawili na Cyprian John.

SOMA NA HII  FAMILIA YAPINGA MAHAKAMANI WOSIA WA MENGI, MAZITO YAIBUKA